"Walinifanya nisiwa'miss watoto wangu!” Rosie alia kwikwi akieleza upendo kwa watoto wa mwajiri wake

"Walijaza ule utupu niliokuwa nikihisi nilipokuwa mbali na watoto wangu. Ninawapenda sana tu,” Rosie alisema akilia.

Muhtasari

•“Maria na Kattie, Mama Rosie anawapenda sana. Na niwa’miss sana,” Rosie alisema na kuangua kilio cha kihisia.

•Rosie alisema kuwa anatumai siku moja watoto wa mwajiri wake watapata fursa ya kutembelea familia yake nchini Keny

Bi Roseline Atieno
Image: HISANI

Mwanadada wa Kenya anayevuma kwenye mitandao ya kijamii, Bi Roseline Atieno Oyola almaarufu Nanny Rosie alizidiwa na hisia alipokuwa akieleza kuhusu upendo wake mzito kwa watoto wa mwajiri wake.

Katika mahojiano na Presenter Ali, mama huyo wa watoto watatu alifunguka kuhusu jinsi anavyoipenda familia hiyo ya Lebanon ambayo amekuwa akiishi nayo kwa miaka miwili iliyopita na jinsi anavyowa’miss watoto ambao amekuwa akiwatunza.

“Maria na Kattie, Mama Rosie anawapenda sana. Na niwa’miss sana,” Rosie alisema na kuangua kilio cha kihisia kisichozuilika.

Akizungumzia kile anachokosa zaidi kuhusu watoto wa mwajiri wake, alisema, “Nina’miss tu jinsi nilivyokuwa nikiwatunza. Walinifanya nisiwa’miss sana watoto wangu. Walijaza ule utupu niliokuwa nikihisi nilipokuwa mbali na watoto wangu. Ninawapenda sana tu.”

Uhusiano mkubwa ambao mwanadada huyo anayetoka Bondo katika Kaunti ya Siaya anao na familia ya Lebanoni ambayo amekuwa akifanyia kazi ulidhihirika waziwazi katika mahojiano hayo kwani hakuweza kuwazungumzia bila kumwaga machozi.

Rosie alisema kuwa anatumai siku moja watoto wa mwajiri wake watapata fursa ya kutembelea familia yake nchini Kenya na kuona jinsi wanavyoishi.

"Ningependa waje kukutana na watoto wangu pia," alisema.

Katika mahojiano hayo, Rosie alitaja kipindi  cha kihisia cha wakati akiondoka Lebanon kama wakati wa huzuni zaidi maishani mwake.

Alisema alijisikia vibaya sana kuwaacha wanandoa ambao amekuwa akiwafanyia kazi tangu Oktoba 2021 pamoja na watoto wao wanne wadogo ambao amekuwa akiwatunza.

"Ilikuwa wakati wa huzuni zaidi maishani mwangu. Ilijawa na hisia tofauti kwa sababu kwa upande mmoja nilifurahi kuja kukutana na familia yangu na kwa upande mwingine nilikuwa na huzuni kwa sababu nilikuwa naacha watoto ambao nimeishi nao kwa miaka miwili,” Rozzie alisema.

Mfanyikazi wa nyumbani huyo pia alifunguka kuhusu uhusiano mzuri na muungano thabiti kati yake na watoto wa mwajiri wake.

Alisema alijisikia kukaribishwa sana alipokuwa na familia ya Lebanon kwani wote walimtendea vyema na walithamini kazi nzuri aliyowafanyia.

“Hapo nilijisikia kuwa nyumbani. Tofauti pekee ni mimi nilikuwa nalipwa. Ninawapenda watoto kwa sababu wanathamini kazi yangu na wananipenda kwa hilo. Walikuwa wakinichukulia kama mzazi wao,” alisema