Mchekeshaji maarufu wa Kenya Vincent Mwasia Mutua almaarufu Chipukeezy amefichua kuwa yeye na mwanasholaiti aliyeuawa, Starlet Wahu walikuwa marafiki.
Wakati akishiriki mazungumzo na Mwafreeka kwenye podikasti ya ‘Iko Nini’, mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show alifichua kwamba alipata kujuana na Wahu baada ya kukutana kupitia mitandao ya kijamii.
Alizungumzia jinsi mrembo huyo mwenye umri wa miaka 26 alivyomsaidia kumfikia kaka yake, Nabii Victor Kanyari na kuandaa mahojiano naye.
“Cha kusikitisha zaidi ni kuwa namjua huyo msichana. Alinitambulisha kwa Kanyari. Kuna mahojiano nilifanya ya Kanyari iko kwa channel yangu,” Chipukeezy alisimulia.
Mchekeshaji huyo aliendelea kufichua jinsi alimtafuta marehemu Wahu wa kwanza, akidokeza kuwa alikuwa na nia ya kimapenzi alipokuwa akichuku hatua ya kuwasiliana naye.
“Nakumbuka wakati moja Kanyari alivuma kama anaskiza ngoma ya kuburudisha akitoka mahali huko Machakos kama huyo msichana anamrekodi. Nilimtumia ujumbe nikamwambia naweza taka kuu.. sina uhakika ni Kanyari nilikuwa natafuta ama ni yeye. Niliingia kwa hiyo DM nikamwambia nataka kumhoji Kanyari,” alisema.
Aliongeza, “Ilikuwa nikimkosa Kanyari, sitakosa dada yake. Alikuwa wa usaidizi sana, alinipatia namba ya Kanyari. Kanyari akakuja nyumbani, kipindi cha pili cha Chipukeezy TV, nilimhoji Kanyari."
Chipukeezy aifichua kuwa aliendelea kuwasiliana na marehemu dadake nabii Kanyari hata baada ya mahojiano.
"Tuliendelea kuongea mara moja lakini maisha yakachukua mkondo tofauti yeye nikawa namuona kwenye mitandao ya kijamii," alisema.
Mchekeshaji huyo maarufu alisema kuwa kifo cha Wahu kilimshtua sana akieleza kwamba mauaji hayo yalikuwa ya kinyama na hakustahili kufa.
Mwili wa marehemu Wahu uligunduliwa siku ya Alhamisi asubuhi katika chumba cha ghorofa ya nne cha AirBnB ya Papino Apartments kilichoko katika mtaa wa South B katika Jiji la Nairobi. Hii ilikuwa baada ya mlinzi kuripoti kumuona mshukiwa, John Matara, akikimbia eneo la tukio.
Katika taarifa yao ya Jumapili jioni, DCI ilithibitisha kuwa mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 34 kwa sasa yuko mikononi mwa polisi na uchunguzi wa mauaji hayo unaendelea. Wapelelezi pia waliwasihi manusura wengine wa chuki ya mshukiwa kujitokeza na kuripoti masaibu yao.
"Wakati uchunguzi wa mauaji ya kinyama ya mwanasosholaiti Starlet Wahu Mwangi mwenye umri wa miaka 26 ukiendelea huku mshukiwa mkuu John Matara akiwa chini ya ulinzi wa polisi, DCI inawaomba waathiriwa na manusura wa uhasama wa mshukiwa kuripoti masaibu yao katika Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Eneo la Nairobi au kituo cha polisi cha karibu,” DCI ilisema kwenye taarifa.
DCI iliripoti kuwa Matara alizuiliwa katika Kituo cha Industrial Area baada ya kukamatwa katika Hospitali ya Mbagathi jijini Nairobi ambapo alikuwa akitafuta matibabu kutokana na majeraha kidogo ya mkono na mguu. Alikamatwa pamoja na rafiki yake wa miaka 25, Anthony Nyongesa ambaye alikuwa akimsaidia hospitalini.
Wapelelezi walidai kuwa mshukiwa huyo ni mnyanyasaji wa kimapenzi ambaye anaweza kuwa sehemu ya genge linalolenga wanawake kwenye tovuti za uchumba.
"Uchunguzi kwa sasa unaelekeza kwa uwezekano wa mkosaji wa kingono ambaye hufanikiwa kwa kuwahadaa waathiriwa wake, na ambaye anaweza kuwa sehemu ya wahalifu wanaolenga wanawake kwenye tovuti za uchumba na Programu zingine za mitandao ya kijamii," DCI ilisema.
Waliongeza, "Tunapopongeza wale ambao wamechukua hatua ya ujasiri ya kuripoti matukio yao mabaya na Matara na/au wanachama wa genge lake linaloshukiwa, tunawahimiza mashahidi zaidi wa ukatili na mashambulizi ya kutisha kujitokeza na kurekodi taarifa na wapelelezi wetu. .”