Mchekeshaji na mburudishaji David Oyando almaarufu Mulamwah ameendelea kukejeli kitendo cha mzazi mwenzake Caroline Muthoni kubadilisha jina la binti yao.
Kuelekea mwisho wa mwaka jana, muigizaji Carol Muthoni ambaye ni maarufu kwa jina la Carrol Sonnie alifichua kuwa amebadilisha rasmi jina la bintiye na kufuta jina la babake.
Wakati akiwashirikisha mashabiki katika kipindi cha Maswali na Majibu, alifunguka kuhusu jinsi alivyoamua kuondoa jina la ukoo la baba kutoka kwa jina la binti yao. Alieleza kuwa bintiye haitwi tena Keilah Oyando lakini sasa anajulikana kama, Keilah Khloe Wangoi Muthoni.
"Keilah anaitwa aje apart from Keilah Khloe ama zote ni English names?" Mtumiaji mmoja wa Instagram mwenye shauku alimuuliza Sonnie.
Wakati akijibu swali hilo, alimshukuru shabiki huyo kwa kuuliza akisema swali hilo lilimpa nafasi kubwa ya kufafanua kuhusu mabadiliko hayo.
"Hapana, zote si majina ya Kiingereza anaitwa Keilah… Tafadhali hakikisheni, blogu zinakuja hivi karibuni, pigeni screenshot ya hii. Keilah anaitwa Keilah Khloe Wangoi Muthoni. Asante sana kwa swali hilo," mama huyo wa binti mmoja alisema.
Kwa hakika, habari hizo zilimfikia Mulamwah ambaye alikejeli kitendo hicho kwa mara ya kwanza kwenye video ya YouTube iliyochapishwa kwenye chaneli ya Ruth K siku chache zilizopita.
Wakati Mulamwah alikuwa akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram siku ya Alhamisi asubuhi, shabiki mmoja alimtania mchekeshaji huyo akimfahamisha kuwa bintiye sasa ana jina tofauti.
"Kyla Oyando sasa ni muthoni waithera," shabiki huyo aliandika.
Baba huyo wa binti mmoja alijibu maoni ya shabiki kwa emoji za kicheko, kuelezea hisia zake kuhusu hali hiyo.
Aliambatanisha emoji hizo na video ya YouTube yake na Ruth K wakishiriki majadiliano kuhusu jina la mtoto wao, ambapo mchekeshaji huyo alikejeli kwa mara ya kwanza kitendo cha Carol Sonnie cha kubadilisha jina.
Katika video hiyo, msanii huyo alisikika akimuonya mpenzi wake wa sasa kuhusu hatua ya kubadilisha jina la mtoto baada ya uhusiano kuvunjika.
"Na hii mchezo wako hii, mtu anapea mtoto jina, baadaye huku unakuja kubadilisha, mi staki hio mchezo,” alisema Mulamwah.
Aliongeza, "Unapee mtoto majina baadaye unaskai tena ni Clinton, sijui nani, sijui nani. Hmmm.”
Ruth alijibu "Bora mtoto habadiliki, jina ni jina."