Mamake Diamond akanusha mwanawe Tanasha kuhamia Tanzania, afichua umri watakaomchukua

Mama Dangote alifichua kuwa Naseeb Jr tayari amerejea Kenya pamoja na mama yake, Tanasha Donna.

Muhtasari

•Alieleza kuwa Naseeb Jr alihamia Tanzania kwa muda kwani mamake alikuwa na majukumu ya kazi katika nchi hiyo jirani.

•Alibainisha kuwa Naseeb Jr ataendelea kukaa na mama yake Tanasha Donna kwa kuwa bado ni mdogo sana kutenganishwa naye.

Diamond Platnumz, Mama Dangote na Naseeb Jr
Image: INSTAGRAM// MAMA DANGOTE

Mama wa mwimbaji wa Bongo Diamond Platnumz, Bi Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote ameweka wazi kuwa mtoto wa mwanawe na Tanasha Donna, Naseeb Jr hajahamia Tanzania.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Wasafi Media, mke huyo wa Uncle Shamte alifichua kuwa Naseeb Junior tayari amerejea nchini Kenya pamoja na mama yake Tanasha Donna.

Alieleza kuwa mvulana huyo mwenye umri wa miaka minne alihamia Tanzania kwa muda mwaka jana kwani mama yake alikuwa na majukumu ya kazi katika nchi hiyo jirani.

“Naseeb Jr haishi Tanzania. Mama yake alikuja kikazi, kamaliza kazi kisha kaondoka. Junior yuko kwao Kenya, kwa mama yake. Sio kwao Tanzania, yuko kwa mama yake Kenya. Ashaondoka muda sasa,” Mama Dangote alisema.

Huku akijibu kuhusu kwa nini mtoto wa mwisho wa Diamond alionekana kujiunga na shule ya Tanzania miezi kadhaa iliyopita, alieleza kuwa shule aliyojiunga nayo Naseeb Jr katika nchi hiyo jirani ni tawi la shule hiyo hiyo anayosoma nchini Kenya.

“Shule aliyosoma hapa, na aliyosoma Kenya ndiyo hiyo. Kaingizwa hapa ndio ili asikae mtoto anacheza tu bila kusoma. Ndo ikabidi ameingizwa hapa, alipotoka hapa kuendelea kule. Hakai hapa,” alieleza Mama Dangote.

Aliongeza, “Hapa (Tanzania) ndio kaanza shule lakini kwa sababu shule ya hapa na ya kule (Kenya) ni sawa . Ndio maana aliingizwa hapa. Mama yake alivyomaliza kazi, wameondoka. Mama yake alikuja kikazi.”

Mamake Diamond Platnumz alibainisha kuwa Naseeb Jr ataendelea kukaa na mama yake Tanasha Donna kwa kuwa bado ni mdogo sana kutenganishwa naye.

Hata hivyo alibainisha kuwa baada ya mvulana huyo atakapofikisha umri wa miaka saba, anaruhusiwa hata kukaa na familia yake nyingine nchini Tanzania.

“Watoto wanakaa kule, lakini wanarudi Tanzania. Tukiwataka hata kesho, wakitoka shule wanakuja. Wakiwa likizo lazima waje wakimaliza likizo wanarudi. Lakini wakifikisha miaka saba wanarudi hapa Tanzania ndio kwao, kwa baba yao,” alisema.

Mama Dangote hata hivyo alieleza kuwa mwanawe na a wazazi wenzake ndio watatoa uamuzi kuhusu mahali watoto hao watakaa.

“Baba na mama watasikilizana kama hivi hapa, wakitaka watakaa. Kama watataka wakae huko ni sawa. Siwezi kusema watakuja kukaa Tanzania, sio hivyo. Msininukuu. Nimeongea tu,” alisema