Staa wa Bongofleva, Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz ametangaza hadharani kuwa sasa yuko single na kuwaacha maelfu ya mashabiki wake katika mshangao.
Diamond alitoa tangazo hilo Jumatano usiku, siku chache baada ya mama yake, Sanura Kassim maarufu Mama Dangote kurekodiwa akisema kuwa bosi huyo wa WCB hajamtambulishia mwanamke yeyote kama mchumba wake.
Katika mahojiano ya hivi majuzi na Wasafi Media, Mama Dangote aliweka wazi kuwa hafahamu kuhusu uhusiano wowote kati ya mwanawe na msanii wake Zuhura Othman almaarufu Zuchu ambaye kwa muda mrefu amekuwa akidaiwa kuwa mpenzi wake.
"(Diamond) hajawahi kuniletea Zuchu eti anataka kumuoa. Mimi kwanza najua Zuchu ni msanii wake," Mama Dangote alisema.
Mamake Diamond alisema hatambui uhusiano wa waimbaji hao kwani hakuna hatua yoyote ya kuelekea kwenye ndoa ambayo imechukuliwa.
"Kusema eti Zuchu ni mchumba wake sijui, kwa sababu mimi sijapeleka mahari kwa kina Zuchu wala barua. Zuchu namjua ni msanii wake.
Kila siku tuko naye sijui,najua ni msanii. Mimi ninachojua mchumba ni yule ambaye unapeleka barua na mahari." alisema.
Aliendelea kuutaja uhusiano wa mwanawe na Zuchu kuwa wa ‘kuchezeana’ huku akibainisha kuwa si wa kweli.
“Kama mtu hajatoa barua, ni kutembea tu. Hiyo inaitwa kuchezeana. Huyo (Zuchu) sio mchumba, huyo ni mwanamke tu,” Mama Dangote alisema.
Aidha, alibainisha kuwa Zuchu si mwanamke wa kwanza kuhusishwa kimapenzi na mwanawe kwani amekuwa akidaiwa kutoka na wanawake wengine wengi waliowahi kuonekana naye katika siku za nyuma.
"Mimi najua mchumba Yule aliyeleta mahari," alisema.
Siku ya Jumatano usiku, mwanamuziki Diamond Platnumz aliweka wazi kuwa hana uhusiano wa kimapenzi na mwanamke yeyote.
“Kuanzia leo ningependa niwatangaze rasmi kuwa I AM SINGLE, sidate wala sina mahusiano na mwanamke yeyote,” Diamond alisema kupitia Instagram.
Staa huyo wa bongofleva aliendelea kuwasihi mashabiki kuacha kumwekea mwanamke yeyote kama mpenzi wake akisema kuwa yeye mwenyewe atakuwa wa kwanza kutangaza atakapoingia kwenye uhusiano.
“Hivyo nisiwekewe mwanamke yeyote kama mwanamke wangu, itakapotokea kudate ama kuwa na mahusiano nitawajuza ama kutambulisha kama jinsi huwa nafanya,” alisema.
Diamond alitoa tangazo hilo kupitia instastori zake lakini akafuta baadaye.