Karen Nyamu azungumzia kuhuzunishwa na ziara ya Samidoh ya Marekani aliko Edday Nderitu

Samidoh yuko nchini Marekani kwa sasa ambapo amepata nafasi ya kukutana na Edday Nderitu na watoto wao.

Muhtasari

•Karen Nyamu amebainisha kuwa hajavunjika moyo wala kupatwa na wasiwasi kufuatia ziara ya mpenzi wake Samidoh nchini Marekani.

•Bi Nyamu alishangaa jinsi watu walivyotarajia angeitikia Samidoh kuwatembelea watoto wake wengine nchini Marekani.

Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU

Seneta wa kuteuliwa Karen Njeri Nyamu amebainisha kuwa hajavunjika moyo wala kupatwa na wasiwasi kufuatia ziara ya mpenzi wake Samidoh nchini Marekani.

Wakati akimjibu mwanamtandao mmoja chini ya moja ya machapisho yake ya Facebook, mama huyo wa watoto watatu alisema kwa ujasiri kwamba mwimbaji huyo wa Mugithi alitembelea nchi hiyo ya Magharibi kuwaona watoto wake, jambo ambalo haliwezi kumtia wasiwasi.

Shabiki mmoja alitaka kujua ikiwa Bi Nyamu alikuwa amevunjwa moyo na suala la mpenzi wake kukutana na aliyekuwa mke wake, Edday Nderitu.

"Je! Kuvunjika moyo kunakupeleka vipi katika maisha haya?" shabiki mmoja alimuuliza Karen Nyamu.

Katika majibu yake, seneta huyo wa kuteuliwa alishangaa jinsi watu walivyotarajia angeitikia Samidoh kuwatembelea watoto wake wengine nchini Marekani.

“Hehehe kutembelea watoto ni kitu inawapenga heartbreak ama nafaa nifurahi. Sasa sitakuwa najitetea mkiniona na yeye kila saa kuniambia nilifanya atupe watoto,” alijibu Bi Nyamu.

Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Haya yanajiri huku mwanamuziki Samidoh akiendelea kufurahia muda na watoto wake watatu na aliyekuwa mke wake, Edday Nderitu nchini Marekani. Edday na watoto wake wamekuwa Marekani kwa miezi michache iliyopita tangu alipoachana na mwimbaji huyo wa Mugithi mapema mwaka jana kwa sababu ya migogoro ya ndoa.

Binti mkubwa wa Samidoh, Shirleen Muchoki mnamo Jumatatu alithibitisha kwamba mwimbaji huyo maarufu wa Mugithi yuko pamoja nao nchini Marekani.

 Shirleen alithibitisha ufichuzi wa awali wa seneta Nyamu ambaye alitangaza habari kuhusu ziara ya Samidoh mwishoni mwa wiki jana katika moja ya posti zake.

Wakati akimjibu shabiki wake mmoja katika moja ya machapisho yake ya hivi majuzi kwenye mtandao wa Facebook, seneta huyo wa kuteuliwa alifichua kuwa Samidoh alienda Marekani kuwaona watoto wake. Pia alitumia fursa hiyo kubainisha wazi kwamba hakutakuwa na tatizo lolote kama mwimbaji huyo wa Mugithi ataamua kusuluhisha mambo na mke wake wa kwanza, Bi Edday Nderitu..

"Yeye (Samidoh) yuko pale tunapozungumza kuwaona watoto. Eddy pia akirudi kwa mix tumeshare miaka mingi sana kwa amani hatawahi kuwa tatizo,” Karen Nyamu alisema Ijumaa.

Zaidi ya hayo, aliweka wazi kuwa hatajiunga na Samidoh na familia yake nyingine nchini Marekani kwa kuwa ingeharibu mambo, kinyume na matakwa yao.