Sababu ya kuhuzunisha kwa nini Jemutai anachukua mapumzika kutoka kwa mitandao ya kijamii

Mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show alifichua kuwa mmoja wa watoto wake hajisikii vizuri.

Muhtasari

•Jemutai alionyesha mwanawe akipokea matibabu kuwabainishia mashabiki wake kwa nini alikuwa akichukua hatua hiyo kuu.

•Jemutai ni mama wa watoto wawili ambao wote aliwapata na mchekeshaji mwenzake Herman Kago almaarufu kama Profesa Hammo.

Image: INSTAGRAM// JEMUTAI

Mchekeshaji mashuhuri wa Kenya Stella Bunei Koitie almaarufu Jemutai ametangaza kuwa atapumzika kutoka kwa mitandao ya kijamii. 

Katika taarifa fupi siku ya Ijumaa asubuhi, mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show alifichua kuwa mmoja wa watoto wake hajisikii vizuri.

 Alionyesha video ya mwanawe akiwa amelala kwenye kitanda cha hospitali akipokea matibabu kuwabainishia mashabiki wake kwa nini alikuwa akichukua hatua hiyo kuu.

“Mtoto wangu hajisikii vizuri. Nachukua mapumziko, tuonane hivi karibuni,” Jemutai alisema chini ya video hiyo aliyoichapisha kwenye mtandao wa Instagram. 

Hata hivyo, hakufichua muda ambao mapumziko yake yatachukua.

Jemutai ni mama wa watoto wawili ambao wote aliwapata na mchekeshaji mwenzake Herman Kago almaarufu kama Profesa Hammo. Wawili hao walikuwa kwenye uhusiano wa siri kwa miaka kadhaa kabla ya mzozo wa kimalezi  kufichua yote mwaka wa 2021.

Kwenye mahojiano ya 2022 hata hivyo, Profesa Hammo alikana ndoa na mama huyo wa watoto wake wawili.  

Akiwa kwenye mahojiano na Tuko Extra, Hamo alieleza kuwa uhusiano wake na Jemutai ni uzazi tu ila sio ndoa.

Mchekeshaji huyo alisema waliafikiana na Jemutai kushirikiana katika malezi ya watoto wao wawili baada ya ndoa kushindikana.

"Mimi na Jemutai tunalea watoto tu pamoja. Niko na mke na Jemutai ambaye tunalea watoto pamoja. Baaada ya kushiriki mazungumzo tuligundua kuwa kuna mambo ambayo hatuwezi kubadilisha. Lakini kuna kitu tulicho nacho, watoto wazuri. Badala ya kufanya mambo ambayo yameshindikana, tuliona kuna kitu ambacho kinafanya kazi, tuko na watoto. Tulikubaliana kuwalea," Hamo alisema.

Aliweka wazi kuwa mkewe hana tatizo lolote kwake kushirikiana na Jemutai katika malezi  ya watoto wao na amekuwa akiunga mkono mpango huo.

Hamo alisema kuwa hajamkazia Jemutai kwa namna yoyote ile na amempa uhuru wa kuishi maisha yake jinsi atakavyo bila kumfuatilia.

"Kila mtu anajua nafasi yake. Najua jinsi ya kusawazisha majukumu yangu, najua jinsi ya kuwa na watoto wangu. Najua namna ya kuwaongelesha wakati siko karibu. Najua namna ya kupatia Jemutai uhuru wa kuishi maisha yake. Namuunga mkono kikamilifu," Hamo alisema.

Mchekeshaji huyo alisema kuwa mazingira ambayo ameweza kujenga yamempa raha kubwa. Aidha alisisitiza kuwa  anajivunia watoto wake na Jemutai sana.