"Waliniachia mume mzuri!" Esther Musila awashukuru ma-ex wa mumewe Guardian Angel

Bi Musila amewapongeza wasichana wote ambao awali walichumbiana na mwimbaji huyo wa nyimbo za injili na baadaye kumtema.

Muhtasari

•Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 53 alisherehekea kuwa wapenzi wa zamani wa Guardian Angel walimwachia mume mzuri sana.

•Bi Musila alibainisha kwamba Guardian Angel kuja maishani mwake ilikuwa sala ambayo Mungu alijibu.

mnamo siku ya harusi yao Januari 2022.
Esther Musila na mumewe Guardian Angel mnamo siku ya harusi yao Januari 2022.
Image: INSTAGRAM

Mkewe Guardian Angel, Esther Musila amewapongeza wasichana wote ambao awali walichumbiana na mwimbaji huyo maarufu wa nyimbo za injili na baadaye kumtema.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 53 alisherehekea kuwa wapenzi wa zamani wa Guardian Angel walimwachia mume mzuri sana.

“Nawashukuru sana ambao walikuwa tayari wapenzi wake wa zamani, wale walimuacha wakifikiri anateseka sana. Walinipatia mume mzuri sana. Yaani nawashukuru sana. Mlimuacha, yaani big up!,” Bi Musila alisema.

Mama huyo wa watoto watatu wakubwa alibainisha kwamba Guardian Angel kuja maishani mwake ilikuwa sala ambayo Mungu alijibu.

"Mimi naweza kusema kwamba maisha yangu ni kama yalianza baada ya miaka 50. Kwa sababu kila kitu nilitamani, nimepatiwa katika miaka minne," alisema.

Aidha, Bi Musila pia alibainisha kuwa katika maisha yake ya zaidi ya miaka 50, hajawahi kuwa na furaha zaidi ya aliyo nayo kwa sasa.

Alisema kuwa yeye na mumewe wana muungano mkubwa sana na kusema kwamba wao ni marafiki zaidi kuliko wanandoa.

“Yaani ukipata tuko wawili tu kwa nyumba, tuna utoto, utashangaa hawa ni watoto wagani. Nadhani muungano wetu ni mkubwa, sisi ni marafiki zaidi ya kuwa mume na mke. Ukiniona ninang’ara hivi, yaani ni kupendwa,” alisema.

Mhasibu huyo mwenye umri wa miaka 53 alibainisha kuwa yeye na Guardian Angel wana urafiki mzuri sana na wenye nguvu ambao unawaunganisha pamoja.

Pia alifichua kuwa tangu walipoamua kufanya maisha pamoja, wanatumia muda wao mwingi pamoja na ni mara chache huwa mbali na kila mmoja.

“Yaani sisi huwa hatuachani, wakati ambao tunaachana ni labda tu nikienda kazini naye aende kazini. Lakini 99% ya maisha yetu huwa tuko pamoja,” alisema.

Aliongeza, “Ningependa tu kumwambia, yaani mpenzi nakupenda tena sana sana. Kutoka kichwani mwangu hadi kidole cha mguu.”

Aidha, Bi Musila alisifu mapenzi mazito aliyo nayo mume wake Guardian Angel kwake akijigamba kuwa yanamfanya ajihisi mtoto.

Alisema kuwa mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 35 anampenda sana bila masharti, jambo ambalo linampa utimilifu mkubwa moyoni mwake.

“Hata bila kumwambia, yeye (Guardian Angel) anajua nampenda sana sana. Kwa sababu amenipa kutimiza maishani mwangu kupita nilivyotarajia,” Esther Musila alisema.

Aliongeza, “Kwa vile ananipenda, kwa vile ananifanyia, yaani nahisi kama mimi ndiye mtoto kwake sasa. Nimeacha kuwa mama kwa umri wangu. Yaani najiskia kama mimi ni mtoto kabisa kwa sababu ya upendo alio nao kwangu.”