“Wamerudiana?” Picha ya Samidoh akifurahia muda na Edday Nderitu yazua msisimko mtandaoni

Samidoh alikuwa amezuru Marekani hivi majuzi ambapo alikutana na mzazi mwenzake Edday Nderitu na watoto wao.

Muhtasari

•Picha Samidoh akiwa na Edday Nderitu imekuwa ikivuma kwenye mitandao mbalimbali na kuzua hisia mseto.

•Staa huyo wa Mugithi alirejea nchini Kenya hivi majuzi lakini Bi Edday Nderitu na watoto wao watatu waliachwa Marekani.

wakifurahia muda pamoja
Samidoh na Edday Nderitu wakifurahia muda pamoja
Image: FACEBOOK// MOSES MARITE

Picha ya staa wa Mugithi, Samuel Muchoki almaarufu Samidoh akiwa na mzazi mwenzake Edday Nderitu imekuwa ikivuma kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kuzua hisia mseto kutoka kwa watumiaji wa mitandao.

Picha inayowaonyesha wanandoa hao wa zamani wakiwa katika hali ya furaha ilichapishwa kwa mara ya kwanza na meneja wa Samidoh, Moses Marite kabla ya watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii kuisambaza

Mashabiki wa wawili hao wameendelea kueleza kuchanganyikiwa kwao mtandaoni, baadhi wakipendekeza kuwa wazazi wenza hao huenda wamerudiana huku wengine wakipendekeza kwamba huenda walikutana ili kuzungumza kuhusu watoto wao.

Picha hiyo huenda ilipigwa wakati wa ziara ya hivi majuzi ya Samidoh nchini Marekani ambako alienda kuwatembelea watoto wake baada ya miezi mingi ya kuwa mbali nao.

Staa huyo wa Mugithi alirejea nchini Kenya hivi majuzi lakini Bi Edday Nderitu na watoto wao watatu waliachwa Marekani ambako wamekuwa tangu mapema mwaka jana.

Bi Edday Nderitu kwa sasa anaishi nchini Marekani pamoja na watoto wao. Aliondoka nchini mapema mwaka jana na anaonekana tayari kutulia huko vizuri huku watoto wakiwa wameanza shule huko.

Mwezi Julai mwaka jana, Bi Edday Nderitu aliweka wazi kwamba alimuacha mumewe ili awe na mwanamke ambaye alionekana kumtaka zaidi.

"Wacha nifafanue mambo machache ambayo yalishirikiwa mtandaoni na sio sahihi. Siko kwenye ndoa ya wake wengi, kama ilivyoelezwa nilimuacha mume kwa yeyote aliyemhitaji zaidi,” Edday alisema kupitia Facebook.

Aliongeza, "Nilifanya uamuzi wa kujiondoa mimi na watoto wangu kutoka kwa mazingira hayo yenye sumu, haswa binti yangu kijana ambaye kwa bahati mbaya anapokea moja kwa moja tabia isiyoaminika iliyoonyeshwa."

Mara nyingi, Bi Edday Nderitu amesisitiza kwamba hayuko tayari kuwa kwenye ndoa ya wake wangi licha ya mpenzi wa Samidoh, seneta Karen Nyamu kusisitiza kwamba yuko tayari ku'share mume naye.