Hisia nzuri huku Zuchu akiburudika na watoto wake wa kambo

Zuchu alishiriki wakati mzuri na watoto wa Diamond na Zari Hassan mwishoni mwa wiki iliyopita.

Muhtasari

•Video ziliwaonyesha Tiffah Dangote, Prince Nillan, Zuchu na Diamond wakiwa kwenye gari moja ambapo wote walionekana kuburudika.

•Miongoni mwa nyimbo ambazo wanne hao walikuwa wakiimba ni ‘Komando’, ‘Chu’ na Mapoz za Diamond Platnumz mwenyewe.

wakifurahia muda pamoja
Diamond Platnumz, Zuchu, Prince Nillan na Tiffah Dangote wakifurahia muda pamoja
Image: INSTAGRAM

Ilikuwa kipindi kizuri huku malkia wa bongofleva Zuhura Othman almaarufu Zuchu akishiriki wakati mzuri na watoto wa Diamond na Zari Hassan mwishoni mwa wiki iliyopita.

Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ziliwaonyesha Tiffah Dangote, Prince Nillan, Zuchu na Diamond Platnumz wakiwa kwenye gari moja ambapo wote walionekana kuburudika.

Wanne hao walionekana wakicheza densi huku wakiimba pamoja nyimbo tofauti za bongo.

"Hisia nzuri na pops @diamondplatnumz," iliandikwa chini ya baadhi ya video zilizoshirikiwa kwenye ukurasa wa Instagram wa Prince Nillan.

Miongoni mwa nyimbo ambazo wanne hao walikuwa wakiimba ni ‘Komando’, ‘Chu’ na Mapoz za Diamond Platnumz mwenyewe.

Hivi majuzi, Diamond aliashiria fahari yake kubwa baada ya mwanawe Prince Nillan kuhudhuria masomo ya Madrasa ili kupata mafundisho ya Kurani.

Katika ukurasa wake wa Instagram, bosi huyo wa WCB alichapisha video za mtoto huyo wake wa pili akipokea mafundisho ya Kurani kutoka kwa mwalimu wa Kiislamu na akionekana kuyafuatilia vizuri mafundisho hayo.

Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 7 pia alionekana akifundishwa kuomba na Kiarabu, na alionekana kuelewa na kuyafuata vizuri yale aliyokuwa akifundishwa na mwalimu wake.

Kusherehekea maendeleo ya mwanawe katika masomo ya Uislamu, msanii Diamond Platnumz alichapisha video hizo kwenye Instastori zake na kuambatanisha video hizo kwa emoji za moyo, ili kuonyesha upendo.

Takriban miezi miwili iliyopita, Diamond alimtuliza mwanawe baada ya kushindwa kuhudhuria sherehe ya siku yake ya kuzaliwa mnamo Desemba 6.

Katika taarifa yake ya mwezi Disemba bosi huyo wa lebo ya WCB alimtaka mtoto huyo wake wa pili wa mwanasosholaiti Zari Hassan asiwe na wasiwasi kuhusu yeye kutohudhuria sherehe yake kwani anapanga kulipa fidia.

Alisema ili kulipia kukosa karamu zilizopita, atawaandalia tafrija kubwa kijana wa miaka saba na dada yake mkubwa Tiffah Dangote.

“Nimekosa siku yako maalum na ya dada yako mwaka huu mwanangu.. Ila usijali, nitawafanyia wote Birthday Party maalum kwa ajili yako na dada yako mtakapokuja kwa ajili ya mkesha wa mwaka mpya nchini Tanzania!!!,” Diamond alisema kupitia Instagram.

Staa huyo wa bongo fleva aliendelea kumhakikisha mwanaye na Zari kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

"Kumbuka Papa anakupenda sana @princenillan," alisema na kuambatanisha taarifa yake na picha ya mvulana huyo wa miaka saba.