Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amefunguka kuhusu kifo cha mwanawe aliyefariki miaka mingi iliyopita.
Katika taarifa siku ya Jumatatu, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alifichua kwamba mwanawe Retreat Roberts Woody Otieno alifariki akiwa na umri wa miezi minane pekee.
Akothee alibainisha kwamba wakati huo alikuwa bado kijana na hakuwa na pesa za kutafuta matibabu yanayofaa kwa mtoto huyo.
“Eeee yawa wakati mwingine nahisi mwanangu angepona ningekuwa na pesa za kumpeleka hospitali . Kama mama kijana nilifiwa na mwanangu mtanashati akiwa na umri wa miezi 8 🙏Bado nina hakika kwamba Retreat Roberts ingekuwa hai kama ningekuwa mtu mzima, aliyefichuliwa zaidi na pesa za matibabu," Akothee aliandika katika taarifa ya kusikitisha Jumatatu.
Mama huyo wa watoto watano aliendelea kumuomboleza marehemu mwanawe lakini hakutoa maelezo mengi kuhusu kilichomuua.
Alizungumzia tukio hilo la uchungu alipokuwa akisherehekea mafanikio ya matibabu ya mtoto mdogo aliyetambulisjwa kwa jina la Sharon ambaye hakuwa ametembea tangu kuzaliwa miaka mitatu iliyopita.
“Leo tuna habari njema kutoka RFH . SHARON ANATEMBEA AKIFUKUZA WATU NA MAMA SASA INABIDI AMFUKUZE . Sharon ambaye kila mara aliachwa nyumbani wakati watu waliondoka kwenda sehemu zingine 🙏🙏,” alisema.
Katika taarifa yake ya siku za nyuma, Akothee aliwahi kufichua kwamba marehemu Roberts Woody Otieno alikuwa mzaliwa wake wa pili na amezikwa nyuma ya shamba aliyokuwa akiishi pamoja na binti zake, Vesha Awuor, Celine Aggry, Prudence Vanpelt, na aliyekuwa mume wake Jared Okello.
Mwishoni mwa mwaka wa 2022, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alipoteza ambaye angekuwa mtoto wake wa sita baada ya kuharibika kwa mimba.
Septemba mwaka jana, alichapisha video ya kihisia iliyomuonyesha akiwa amemshika mtoto mchanga akijaribu kumtuliza huku akiendelea kushiriki mazungumzo na mama wa mtoto huyo.
Katika taarifa yake, alisema mtoto huyo mdogo alimkumbusha ambaye angekuwa mtoto wake na mumewe Denis ‘Omosh’ Shweizer ambaye alitarajia kujifungua mwezi Julai mwaka jana lakini kwa bahati mbaya akapoteza ujauzito huo Desemba mwaka jana.
“Huyu mtoto amenikumbusha kuwa mtoto wetu angekuwa na mwezi 1 na wiki moja leo. Ilinibidi nimkumbushe mume wangu siku yetu kubwa tarehe 22 Julai,” Akothee alisema.
Wakati huo huo, alikiri kuwa bado hawajui kilichotokea hadi akapoteza ujauzito huo lakini akafichua kuwa bado wanaendelea kujaribu tena.
"Sijui kilichotokea, bado tunajaribu," alisema.