Alikiba na aliyekuwa mkewe, Amina Khalef wamsherehekea mtoto wao

Wazazi wenza hao walikuwa na jumbe nzuri kwa mtoto wao alipofikisha umri wa miaka mitano Jumatatu.

Muhtasari

•Keeyan ambaye ni mtoto wa kwanza wa Alikiba na mrembo huyo wa Kenya aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya tano mnamo Februari 19.

•Bi Amina Khalef pia alishiriki picha sawa na kuomba baraka za Mungu kwa mwanawe.

Alikiba na aliyekuwa mke wake, Amina Khalef
Image: HISANI

Siku ya Jumatatu, staa wa Bongo, Ali Saleh Kiba almaarufu Alikiba na aliyekuwa mke wake Amina Khalef walimsherehekea mtoto wao Keeyan Alikiba mnamo siku yake ya kuzaliwa.

Keeyan ambaye ni mtoto wa kwanza wa Alikiba na mrembo huyo wa Kenya aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya tano mnamo Februari 19 na wazazi wenza hao wawili walikuwa na ujumbe mzuri kwake.

Kwa upande wake, bosi huyo wa King's Music Records alishiriki picha nzuri ya mvulana huyo na kumtakia siku njema ya kuzaliwa.

“Kheri ya siku ya kuzaliwa mwanangu,” Alikiba aliandika.

Bi Amina Khalef pia alishiriki picha sawa na kuomba baraka za Mungu kwa mwanawe.

“Baraka za Mungu na ziwe nawe sikuzote,” aliandika.

Image: INSTAGRAM// ALIKIBA

Alikiba na mkewe huyo wa zamani kutoka Kenya walikuwa wamejaliwa watoto wawili kabla ya ndoa yao kugonga mwamba takriban miaka miwili iliyopita.

Talaka ya staa huyo wa bongo fleva na Bi Amina Khalef  iligonga vichwa vya habari mnamo mwezi Februari mwaka wa 2022

Ombi la talaka liliwasilishwa mahakamani na mwanamke huyo mzaliwa wa Pwani ya Kenya na kusikilizwa kwa miezi kadhaa kabla ya kuamuliwa.

Miezi kadhaa baadaye, mama huyo wa watoto wawili alitangaza kuwa yupo 'huru rasmi', ujumbe ambao ulieleweka kumaanisha kesi ilikuwa imekamilika.

Amina, ambaye sio maarufu sana kwenye mitandao ya kijamii, alipakia picha ya ngome iliyo wazi na ndege akiruka.

Pia alifuta picha zote na AliKiba, zikiwemo zile za harusi yao ya kifahari iliyofanyika mnamo Aprili 2018.

Duru za kuaminika sasa zilisema AliKiba alijaribu kuokoa ndoa yake, ingawa mwishowe juhudi zake zikaambulia patupu.

“Tangu alipoomba talaka, Alikiba amesafiri kwenda Kenya mara nyingi akiwa hajitambui ili kujaribu kurekebisha mambo, lakini Amina alionekana kuwa ameamua,”  chanzo cha habari kilisema.

Kabla ya kudai talaka, inasemekana Amina alimpa mwimbaji huyo nafasi ya kurekebisha mambo, lakini hakufanya hivyo.

"Amina alikuwa ameamua kutulia na kulea familia na Ali," chanzo kilisema.

"Ilifika wakati alihisi kuwa alikuwa akimchukulia kawaida na hakuweza kuvumilia tena. Aliamua kuondoka."