Kimeumana! Mungai Eve na Director Trevor wakatisha uhusiano wa kikazi, mabadiliko yatangazwa

Director Trevor alitangaza kuwa huduma za Mungai Eve hazitahitajika tena.

Muhtasari

•Trevor alitangaza mabadiliko kadhaa makubwa katika kampuni ya Mungai Eve Media ambayo yatatekelezwa Jumanne, Februari 20.

•Director Trevor alitangaza kuwa kampuni hiyo ya habari za mitandaoni itabadilisha jina lake kuwa Kenya Online Media.

wakati wa siku zao za furaha.
Director Trevor na Mungai Eve wakati wa siku zao za furaha.
Image: INSTAGRAM// MUNGAI EVE

Wapenzi mashuhuri wa Kenya, Director Trevor na Mungai Eve wameendelea kudokeza kuhusu kusambaratika kwa uhusiano wao huku wawili hao sasa wakiwa hawafanyi kazi tena pamoja.

Siku ya Jumatatu jioni, Director Trevor ambaye jina lake halisi ni Bonaventure Monyancha alitangaza mabadiliko kadhaa makubwa katika kampuni ya Mungai Eve Media ambayo yatatekelezwa Jumanne, Februari 20

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 alitangaza kuwa kampuni hiyo ya habari za mitandaoni itabadilisha jina lake kuwa Kenya Online Media.

"Je, uko tayari? Taarifa rasmi itashuka kesho," Director Trevor alitangaza.

Alifichua kuwa kutakuwa na mabadiliko kwenye chaneli za YouTube za Mungai Eve na Insta Fame zenye jumla ya wafuasi zaidi ya 850,000 pamoja na ukurasa wa Facebook wa Mungai Eve Media wenye takriban wafuasi 874,000

Wakati alipoulizwa ikiwa ataendelea kufanya kazi na mpenzi huyo wake wa muda mrefu, Trevor alisema kuwa huduma zake hazitahitajika tena.

"Hapana! Huduma zake hazihitajiki tena kwenye mifumo ifuatayo, YouTube – wanaofuatilia 754k, wanaofuatilia Insta Fame 104k, Facebook 874k," alisema.

Katika taarifa nyingine, mtaalam huyo wa mitandao ya kijamii alionekana kumrushia vijembe Mungai Eve akidokeza kuwa mrembo huyo mwenye umri wa miaka 23 anafurahia matunda ya mti alioupanda muda mrefu uliopita.

"Kuna mtu ameketi kivulini leo kwa sababu mtu alipanda mti muda mrefu uliopita," aliandika.

Hatua ya hivi punde ya Director Trevor imezidisha tetesi za kuachana kwao ambazo zimekuwa zikivuma kwenye mitandao ya kijamii hivi karibuni.

Katika miezi michache iliyopita, wapenzi hao mashuhuri hawajaonekana sana wakiwa pamoja na vitendo vyao kwenye mitandao ya kijamii na hadharani vimedokeza kuwa mambo si mazuri kati yao.

Licha ya Director Trevor kutoa matangazo ya maendeleo mapya, Mungai Eve hata hivyo bado hajazungumza kuihusu.