Flaqo aweka mambo wazi kuhusu mpenzi wake Keranta kuwa mjamzito

Mchekeshaji Flaqo Raz kwa mara nyingine amelazimika kujibu tetesi za mpenzi wake Keranta kuwa mjamzito.

Muhtasari

•Kumekuwa na tetesi nyingi kwenye mitandao ya kijamii zinazodai kuwa wapenzi hao wanatarajia mtoto wao wa kwanza pamoja.

•Flaqo aliweka wazi kuwa hatarajii mtoto na kuwataka mashabiki wao kuacha kufuata uvumi.

Flaqo na mpenzi wake Keranta
Image: HISANI

Mchekeshaji Erastus Ayieko Otieno almaarufu Flaqo Raz kwa mara nyingine amelazimika kujibu tetesi za mpenzi wake Winnie Keranta kuwa mjamzito.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita, kumekuwa na tetesi nyingi kwenye mitandao ya kijamii zinazodai kuwa wapenzi hao mashuhuri wanatarajia mtoto wao wa kwanza pamoja.

Katika taarifa yake ya Jumatano asubuhi, Flaqo alifichua kuwa wamekuwa wakipokea jumbe nyingi za pongezi kutoka kwa mashabiki wanaoamini kuwa Keranta ni mjamzito. Hata hivyo alisisitiza kuwa mpenzi wake hana mimba na hawatarajii mtoto.

"Imekuwa zaidi ya mwaka 1 na nusu bado napata pongezi kila siku hata kutoka kwa watu wanaonifahamu kibinafsi, wasionijua binafsi na hata wanafamilia," Flaqo alisema kupitia mtandao wa Instagram.

Aliambatanisha taarifa yake na screenshot mbili za majibizano yake na watu asiotambulisha ambao walimpongeza wakidai kuwa wanatarajia mtoto.

Aliweka wazi kuwa hatarajii mtoto na kuwataka mashabiki wao kuacha kufuata uvumi.

“Huu nabaki kushangaa, hii mimba kwani iko benki gani inagain interest na mimi ndio nilipoteza interest?? Watu waache hii mambo ya uvumi buana.. Sitarajii mtoto yeyote,” alisema.

Alibainisha kuwa kuna blogu kadhaa zimekuwa zikieneza madai yasiyo ya kweli kuhusu mpenzi wake kuwa mjamzito.

Image: INSTAGRAM// FLAQO RAZ

Mwezi Oktoba mwaka jana, Keranta alijibu uvumi kwamba ana ujauzito wa mtoto wake wa kwanza akisema kwamba hata hana mpango wa kupata mtoto hivi karibuni.

"Nafikiri watu wanapaswa kuacha kunilazimisha mimba. !!!Siko popote karibu na mipango yangu 100% Keranta ameongeza uzito !!!Waniache tu inazidi kuwa nyingi," alisema.

Flaqo alithibitisha kuwa anachumbiana na mtayarishaji wa maudhui Keranta mnamo Februari mwaka jana walipokuwa wakiadhimisha miaka mitatu pamoja.