Mtangazaji wa redio wa zamani Andrew Kibe amefichua kuwa mtayarishaji wa maudhui Mungai Eve aliomba kufanya mahojiano ambayo wawili hao walikuwa nayo siku chache zilizopita.
Wakati akihojiwa na waandishi wa habari za mtandaoni hivi majuzi, mtumbuizaji huyo aliyezingirwa na utata mwingi ambaye alikuwa akiishi Marekani kwa miezi kadhaa alisema alikubali kufanyiwa mahojiano na Eve baada ya kuomba kikao naye.
Alisema alikossa kufanya mahojiano na aliyekuwa mpenzi wa Eve, Director Trevor, ambaye sasa anaendesha ‘Kenyan Online Media’ kwani hakuomba.
“Trevor hakunilipa, mimi sina chuki. Mimi nasema Trevor alikuwa anilipe, hakunilipa, kwa nini nifanye mahojiano bure. Je, nakaa mjinga?,” Andrew Kibe alisema.
Alipoulizwa iwapo Mungai Eve alimlipa kwa mahojiano, alionekana kusita kujibu swali hilo na kusema, “Sisemi hivyo (kwamba Mungai Eve alinilipa), ninasema tu Trevor hakunilipa.”
Aliongeza, “Trevor hakuomba mahojiano, bali Mungai Eve aliomba mahojiano.. Eve alipokuja na kuomba mahojiano, nilikubali.”
Mtangazaji huyo wa zamani wa redio hata hivyo aliweka wazi kuwa hatakubali kufanya mahojiano na ex wa Mungai Eve iwapo ataomba katika siku zijazo.
“Zii, sipendi vibe ya huyo kijana,” alisema.
Kibe pia alidokeza kuwa watayarishaji wa maudhui nchini Kenya wamekuwa wakisusia kumwomba mahojiano ilhali yuko tayari kukubali maombi yao.
“Shida yenu ni punitics, mko na punitics na karoho mbaya, karoho plaque,” aliwaambia waundaji wa maudhui.
Mungai Eve alipata fursa ya kushangaza ya kumhoji Andrew Kibe siku chache zilizopita na mahojiano yao yalikuwa ya kwanza kupakiwa katika chaneli yake mpya ya YouTube.
Mahojiano hayo yaliwashangaza wengi kwani katika siku za nyuma, mtangazaji huyo wa zamani wa redio alitofautiana waziwazi na Eve na Trevor walipokuwa wakichumbiana.
Mwezi uliopita, Director Trevor ambaye jina lake halisi ni Bonaventure Monyancha alitangaza mabadiliko kadhaa makubwa katika kampuni ya Mungai Eve Media ambayo yalianza kutekelezwa Jumanne, Februari 20
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 alitangaza kuwa kampuni hiyo ya habari za mitandaoni ilibadilisha jina lake kuwa Kenya Online Media.
"Je, uko tayari? Taarifa rasmi itashuka kesho," Director Trevor alitangaza.
Alifichua kuwa kungekuwa na mabadiliko kwenye chaneli za YouTube za Mungai Eve na Insta Fame zenye jumla ya wafuasi zaidi ya 850,000 pamoja na ukurasa wa Facebook wa Mungai Eve Media wenye takriban wafuasi 874,000
Wakati alipoulizwa ikiwa ataendelea kufanya kazi na mpenzi huyo wake wa muda mrefu, Trevor alisema kuwa huduma zake hazitahitajika tena.
"Hapana! Huduma zake hazihitajiki tena kwenye mifumo ifuatayo, YouTube – wanaofuatilia 754k, wanaofuatilia Insta Fame 104k, Facebook 874k," alisema.