Ommy Dimpoz amuaibisha Alikiba jukwaani kuhusu Kiingereza chake kibovu

Dimpoz alisema alishindwa kumrekosoa Alikiba katika siku za nyuma kwani tayari alikuwa staa mkubwa kuliko yeye.

Muhtasari

•Ommy Dimpoz alimkosoa kwa utani  Alikiba jukwaani kuhusu Kiingereza chake kibovukatika siku za nyuma.

•Alibainisha kuwa katika wimbo wao wa ‘Nai Nai’, Alikiba alisema ‘In my mind’ ilhali alitakiwa kusema ‘On my mind’.

Alikiba na Ommy Dimpoz jukwaani
Image: HISANI

Mwanamuziki mashuhuri wa Tanzania Omary Faraji Nyembo almaarufu Ommy Dimpoz mnamo siku ya Jumamosi usiku alimkosoa kwa utani msanii mwenzake wa bongo fleva Alikiba jukwaani kuhusu Kiingereza chake kibovu katika siku za nyuma.

Dimpoz alikuwa akimpongeza bosi huyo wa Kings Music Records kwa kuanzisha vituo vyake vya habari na kusimulia safari yao pamoja alipomkosoa kuhusu uchaguzi wake mbaya wa maneno ya Kiingereza katika wimbo ambao waliufanya miaka kadhaa iliyopita.

Alibainisha kuwa katika wimbo wao wa ‘Nai Nai’, Alikiba alisema ‘In my mind’ ilhali alitakiwa kusema ‘On my mind’.

“Katika ule wimbo wetu wa kwanza ‘Nai Nai’, Bwana Ali tumefika studio akaanza “Nai Nai, ukinikubali sikatai jua you’re always in my mind”. Nikashindwa hiki kiingereza cha Kariakor.., ni ‘In my mind’ ama ‘On my mind’?” Ommy Dimpoz alimtania Alikiba jukwaani.

Muimbaji huyo alibainisha kuwa wakati wanarekodi wimbo huo alishindwa kumrekebisha Alikiba kwa kuwa alikuwa mkubwa kwenye tasnia ya muziki.

“Nilishindwa kumwambia sababu yeye ndiye staa. Lakini nataka nikwambie leo kuongea ukweli, pale ulikoseaa,” alimwambia Kiba huku wageni waliokuwa wamekusanyika kushuhudia uzinduzi wa Crown Media wakicheka kwa nguvu.

Kwa Kiingereza, huwa tunasema kitu kiko "on my mind" wakati kinajaza mawazo yetu - kwamba tunakifikiria sana. Kwa upande mwingine, tunasema kitu kiko "in my mind" kuashiria kwamba tumekumbuka kitu lakini hakijazi mawazo yetu.

Dimpoz pia alimtania bosi huyo wa Kings Music Record kuhusu Crown Media akimwambia aachie kituo hicho chake kipya cha habari kuwa mali ya ‘familia, akionekana kumtupia vijembe Diamond Platnumz anayemiliki Wasafi Media.

Alikiba hata hivyo alikataa ombi la msanii mwenzake akisema, "Apana, hii ni ya kila mtu."

Staa huyo wa bongofleva alizindua vituo vyake vya Crown FM na Crown TV siku ya Jumamosi jioni wakati akisherehekea miaka ishirini katika tasnia ya burudani.

Huku akizungumzia sababu ya kuamua kuzindua vituo vyake vya habari, staa huyo wa bongo fleva alibainisha kuwa redio na tv zimekuwa nguzo kuu katika kujenga taaluma yake ya muziki.

“Media ni chombo chenye nguvu sana, Media ndio iliyonifanya kuwa Alikiba huyu wa leo,” Alikiba alisema wakati wa uzinduzi wa vituo vyake.

Aliongeza, “Ila pia mimi nilikuwa silali bila redio yangu ndogo niliyoletewa zawadi na baba yangu kupigwa muziki. Changamoto nilizopitia na kutatua kuleta suluhisho kwenye media ndivyo ndivyo vimenipa msukumo."

Mwimbaji huyo mkongwe alitangaza kuwa Crown Media haitakuwa na kituo cha redio na tv pekee, bali pia itakuwa na majukwaa ya kidijitali ili kusaidia kufikia mahali ambapo hakuna mipaka na pia huduma ya usimamizi wa hafla ambayo itasaidia kufika pale mashabiki walipo