Rayvanny hatimaye afichua sababu kuu ya kutengana na Diamond

Vanny Boy amefunguka kuhusu kuondoka kwake kutoka lebo ya muziki ya Wasafi (WCB) takriban miaka miwili iliyopita.

Muhtasari

•Rayvanny alisema sababu kuu iliyomfanya aondoke kwenye lebo hiyo inayomilikiwa na mwimbaji Diamond ni kwa kuwa alihitaji uhuru.

•Staa huyo wa bongofleva alifichua kuwa mchakato wa kuondoka Wasafi hadi kujitegemea haikuwa rahisi.

Diamond na Rayvanny
Diamond na Rayvanny
Image: Instagram

Staa wa Bongofleva, Raymond Mwakyusa maarufu Rayvanny amefunguka kuhusu kuondoka kwake kutoka lebo ya muziki ya Wasafi (WCB) takriban miaka miwili iliyopita.

Akizungumza kwenye podikasti ya Imo, bosi huyo wa Next Music Level alisema sababu kuu iliyomfanya aondoke kwenye lebo hiyo inayomilikiwa na mwimbaji Diamond Platnumz ni kwa kuwa alihitaji uhuru.

Alisema alikuwa na uzoefu mzuri wa kufanya kazi na bosi huyo wake wa zamani lakini akabainisha kwamba ilifika wakati alihisi kuwa amefikia kiwango cha kuwa peke yake.

“Nilisainiwa naye (Diamond), nilikuwa chini ya lebo ya Wasafi. Tulifanya mambo mengi pamoja. Tulifanya mambo mengi makubwa pamoja,” Rayvanny alisema.

"Ilifika wakati niliposema, nadhani ni mzima vya kutosha kuhamia kwangu, kujitegemea," aliongeza.

Hata hivyo alifichua kuwa mchakato wa kuondoka Wasafi hadi kujitegemea haikuwa rahisi.

"Ni vigumu. Lakini jambo zuri ni kwamba, tuna mawasiliano mazuri. Kwa sababu kwa kawaida wasanii wanapoacha lebo huwa sio nzuri kila wakati,” alisema.

Msanii huyo wa zamani wa WCB aliipongeza kampuni yake ya usambazaji kwa kusaidia hatua hiyo na akaweka wazi kuwa sasa yuko huru sana.

Aidha, alibainisha kuwa kujitegemea imekuwa changamoto nzuri kwani imemruhusu kujaribu mambo kwa njia yake.

"Ni wewe sasa, ikiwa utashindwa au kushinda, ni juu yako. Ni changamoto nzuri kwangu kujitambua,” alisema.

Rayvanny hatimaye aliondoka rasmi kutoka WCB mnamo Julai 2022 baada ya kufanya kazi chini ya Diamond Platnumz kwa takriban miaka sita.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Next Level Music alitangaza kuondoka kwake kwenye Instagram katika video ya hisia ambapo alisimulia uzoefu wake chini ya lebo hiyo.

“Ni miaka sita tangu tuanze kufanya kazi pamoja, timu yangu, familia yangu WCB Wasafi, upendo, umoja imekuwa nguzo kubwa sana kama timu,” alisema.

Rayvanny aliishukuru label ya Diamond kwa kuwa na mchango mkubwa katika maisha yake ya muziki.

Alisema amefanikiwa kama msanii wa Wasafi.

"Nimejifunza mengi kutoka kwa timu na pia, tumepata mafanikio mengi kama timu. Mmenilea na kukuza talanta yangu," Rayvanny alisema.

Akielezea sababu iliyomfanya aondoke lebo hiyo, Rayvanny alisema anataka kutengeneza fursa zaidi kwa wanamuziki wajao.

“Ni wakati wangu wa kuondoka nyumbani na kuanza maisha mapya, lengo ni kukua na pia ni kutengeneza fursa kwa wasanii wengine, naondoka na wengine kusaidiwa, nitakuwa nasaidia wanamuziki wengine wachanga popote niendako. . Nilisaidiwa kufikia kiwango hiki."

Diamond alimtakia Rayvanny heri akiandika, "RAIS wa NLM! Twendeoooooo!"