logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ni chuo changu pekee wasichana hufuzu wakiwa mabikira – Kasisi mmiliki wa chuo ajigamba

Kasisi alisema itikadi kali, ushoga na wizi wa mitihani ni mambo hayako chuoni kwake.

image
na Radio Jambo

Habari21 March 2024 - 06:29

Muhtasari


• Kwa mujibu wa tovuti ya chuo hicho mitandaoni, kilianzishwa mwaka wa 1999 na tayari kina matawi matatu katika majimbo ya Anambra, Enugu na River.

Rev Fr Emmanuel Edeh

Kasisi ambaye pia ni mwanzilishi wa chuo kimoja nchini Nigeria amezua gumzo mitandaoni baada ya kudai kwamba chuo chake kina upekee wa aina yake kwani ndicho chuo pekee ambacho wanafunzi wasichana hufuzu wakiwa bado mabikira.

Padre huyo kwa jina Emmanuel Edeh, mmiliki na mwanzilishi wa chuo cha Madonna alisema kwa kujipiga kifua Jumatano kwamba wasichana ambao wanaingia katika chuo hicho wakiwa mabikira hufuzu baada ya masomo yao wangali mabikira vile vile.

Katika video hiyo ambayo imezua maswali mengi kuliko majibu, wengi wakihoji anajuaje kuwa wasichana hao hufuzu wakiwa mabikira, mtumishi wa Mungu aliwataka wanaume wanaotafuta wasichana wa kufunga ndoa nao, basi wasitafute kuingine bali waende katika chuo cha Madonna, ila akaonya kwamba hatokubali hilo hadi pale wasichana wa chuo chake watakapofuzu.

“Ni katika chuo hiki pekee ambapo iko wazi kwamba wasichana ambao wanaingia katika chuo hiki kama mabikira humaliza masomo yao wakiwa mabikira. Unaweza ukaingia katika chuo chetu ukiwa bikira na umalize ukiwa bikira,” mtumishi wa Mungu alisema kwa sauti yenye msisitizo.

“Niambieni chuo chochote duniani ambacho kinaweza kudumisha utamaduni wa aina hii. Hii ndio maana watu kutoka London, Ujerumani, Amerika, wakati ninakutana nao, wananiambia, ‘Padre, ninataka kuoa mwanamke ambaye ni bikira, na mara nyingi huwa hawapati hao mpaka pale wanapokuja chuo cha Madonna,” aliongeza.

Ili kufanikisha hili, kasisi huyo alieleza kwamba wanafunzi wote wa chuo hicho wanaishi katika mabweni na hawaruhusiwi kutoka nje ovyo ovyo.

Kasisi huyo wa kanisa Katoliki pia alisema kwamba mambo kama mafunzo ya itikadi kali, ushoga na wizi wa mitihani hayawezi kusikika wala kupatikana katika chuo hicho.

Kwa mujibu wa tovuti ya chuo hicho mitandaoni, kilianzishwa mwaka wa 1999 na tayari kina matawi matatu katika majimbo ya Anambra, Enugu na River.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved