Terence Creative abubujikwa na machozi akimuomboleza Brian Chira (+video)

"Nenda vizuri Chira, mimi ni yatima niliyelelewa na nyanya, hii amenipiga sana," Terence alisema.

Muhtasari

•Mchekeshaji Terence Creative alishindwa kuzuia machozi yake alipokuwa akimuomboleza marehemu Brian Chira.

•Haya yanajiri huku mazishi ya mwanatiktok huyo wa miaka 23 yakiendelea katika kaunti ya Kiambu.

alishindwa kuzuia machozi wakati akimuomboleza Brian Chira.
Terence Creative alishindwa kuzuia machozi wakati akimuomboleza Brian Chira.
Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji na mburudishaji maarufu wa Kenya Lawrence Macharia almaarufu Terence Creative alishindwa kuzuia machozi yake alipokuwa akimuomboleza marehemu Brian Chira.

Siku ya Jumanne asubuhi, alishiriki video iliyomwonyesha akiwa kwenye gari lake huku akisikiliza wimbo wa huzuni wa maombolezo wa Kikuyu.

“Brian Chira, pumzika kwa amani,” Terence alisema kwenye video hiyo na kuendelea kuimba wimbo huo wa maombolezo wa Kikuyu.

Wakati akiendelea kuimba, machozi yalionekana yakitiririka mashavuni mwake bila kujizuia.

Katika sehemu ya maelezo ya video hiyo, mchekeshaji huyo alisema kuwa kifo cha Brian Chira kilimgusa sana kwani wanashiriki hadithi sawa ya malezi.

Alieleza kuwa, sawa na marehemu mwanatiktok huyo, yeye pia ni yatima aliyelelewa na nyanya yake.

"Nenda vizuri Chira, mimi ni yatima niliyelelewa na nyanya, hii amenipiga sana," Terence aliandika.

Aliongeza, "RIP Chira, ulipendwa."

Haya yanajiri huku mazishi ya mwanatiktok huyo wa miaka 23 yakiendelea katika kaunti ya Kiambu.

Mamia ya waombolezaji walikusanyika katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Chuo Kikuu cha Kenyatta Jumanne asubuhi kabla ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika Githunguri, Kiambu.

Waombolezaji walipata kuutazama mwili wa marehemu tiktoker huyo katika chumba cha kuhifadhia maiti kabla ya mazishi ya msafara kuelekea nyumbani kwa nyanya yake kwa mazishi.