"Hajui neno la Kiswahili!" Bahati, Diana Marua walalamikia kuhusu mtoto wao kutojua Kiswahili

Walifichua kuwa, mbali na Majesty, binti yao wa kwanza pia anazungumza Kiswahili kwa lafudhi ya kigeni.

Muhtasari

•Bahati alimuuliza mume wake Bahati kuhusu wasiwasi ambao angeibua mbele ya mwalimu watakapofika shuleni.

•Diana Marua alikubaliana na mumewe akibainisha kuwa mtoto wao Majesty hajui neno lolote la Kiswahili.

Image: YOUTUBE// DIANA MARUA

Wanandoa mashuhuri wa Kenya Bahati na Diana Marua wameibua wasiwasi kuhusu mtoto wao wa pili Majesty Bahati kutoweza kuzungumza Kiswahili.

Wawili hao waliibua suala hilo wakati walipokuwa wakielekea katika shule ya mtoto wao huyo wa kiume kushauriana kuhusu maendeleo yao ya masomo.

"Ni wiki ya mashauriano. Kimsingi ni kujua maendeleo ya mtoi wako. Jinsi anavyoendelea na masomo yake. Alafu pia sisi tunaleta wasiwasi ambao tunakuwa nao na watoto wetu. Ama kama sio hivyo, ni kushukuru tu juhudi wanazofanya walimu wao,” Diana Marua alisikika akisema kabla ya kuingia kwenye lango la shule.

Aliendelea kumuuliza mume wake Bahati kuhusu wasiwasi ambao angeibua mbele ya mwalimu watakapofika shuleni.

“Mbona mtoto wangu hajui Kiswahili, kwa nini anaongea Kizungu tu!” Bahati alijibu.

Diana Marua alionekana kukubaliana na mumewe akibainisha kuwa mtoto wao Majesty hajui neno lolote la Kiswahili.

Bahati alitumia fursa hiyo kufunguka kuhusu siku zake za shule ambapo angeadhibiwa vikali kwa kuongea Kiswahili, Sheng na Kiingereza kibovu.

"Sielewi jinsi mwanangu hajui neno la Kiswahili," mwimbaji huyo alijibu.

Wanandoa hao walifichua kuwa, mbali na Majesty, binti yao wa kwanza pia anazungumza Kiswahili kwa lafudhi ya kigeni.

Hata hivyo hawakuonekana wakimuuliza mwalimu kuhusu suala la kutoweza kwa watoto wao kutumia Kiswahili vizuri.

Baadaye wakiwa shuleni, Bahati na Diana walijaribu kumfanya Majesty aongee neno moja au mawili kwa Kiswahili lakini hakuweza.

"Waambie habari zenu. Waongeleshe Kiswahili," Bahati alimwambia mwanae Majesty ambaye alionekana kutoelewa neno lolote alilokuwa akisema.

Baada ya kufika nyumbani kwao, Bahati alimuomba mwanawe kupiga honi kwa Kiswahili na akafanya hivyo.

Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alionekana kusherehekea kwamba angalau kuna neno la Kiswahili ambalo mvulana huyo alielewa.