Georgina Njenga asherehekea mwezi mmoja bila kunywa pombe

Alisherehekea kuweza kuepuka vishawishi na kuendelea na nia yake ya kuacha vileo.

Muhtasari

•Katika taarifa fupi siku ya Jumapili, mama huyo wa binti mmoja alifichua kuwa yuko katika safari ya kuacha kunywa pombe.

•“Yaani ata jana (Jumamosi) ambalo lilikuwa jaribu rahisi ambalo bado niliepuka. Napanga kufikia miezi mitatu," alisema.

Image: INSTAGRAM// GEORGINA NJENGA

Mtayarishaji wa maudhui mashuhuri wa Kenya Georgina Njenga amesherehekea hatua kubwa maishani mwake, mwezi mzima bila kunywa pombe.

Katika taarifa fupi siku ya Jumapili, mama huyo wa binti mmoja alifichua kuwa yuko katika safari ya kuacha kunywa pombe.

Alisherehekea kuweza kuepuka vishawishi na kuendelea na lengo lake, akibainisha kuwa ana hamu sana ya kufikia miezi mitatu bila kileo.

"Mwezi 1 wa kuacha kutumia pombe na najivunia sana," Georgina alisema kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Aliongeza, “Yaani ata jana (Jumamosi) ambalo lilikuwa jaribu rahisi ambalo bado niliepuka. Napanga kufikia miezi mitatu."

Mpenzi huyo wa zamani wa muigizaji Tyler Mbaya almaarufu Baha alikuwa miongoni mwa mashabiki waliohudhuria tamasha la Raha Fest kwenye bustani ya Uhuru Gardens wikendi iliyotamatika.

Safari ya Georgina ya kuacha pombe inakuja wakati ambapo kuna vita vikali dhidi ya ulevi miongoni mwa vijana, ikiongozwa na naibu wa rais Rigathi Gachagua na mkewe Dorcas Rigathi.

Mwezi uliopita, DP alisisistiza kuhusu vita vyake dhidi ya pombe huku akibainisha kuwa hatua yake haina uhusiano wowote na siasa.

Akizungumza wakati wa mahojiano na Inooro TV, alisema kuwa yeye na mkewe Dorcas Rigathi wamewekeza nguvu zao katika vita dhidi ya dawa hiyo ya kulevya kwani pia wao wamekuwa waathiriwa wa athari zake mbaya.

Rigathi alitumia mahojiano hayo kusimulia kwa hisia kuhusu kifo cha marehemu kakake Jackson Reriani Gachagua ambaye alidai aliuawa na pombe.

“Ndugu yangu Reriani alikuwa mlevi. Nilijaribu kuzungumza naye na kumsihi ‘ndugu yangu tumeachwa wawili tu, nakuomba tafadhali usiniache peke yangu’ lakini hakusikia,” Rigathi alisimulia.

Naibu rais alisema kifo cha aliyekuwa kakake mkubwa kilimuacha katika hali ya huzuni kwani sasa hana ndugu wa kuzungumza naye.

“Sasa nikirudi nyumbani huwa natazama tu makaburi, hakuna wa kuzungumza naye kwa sababu dada zangu walishaolewa. Dada zangu wote wameolewa. Katika nyumba nzima ya Gachagua, mimi ndiye pekee. Kuhusu Reriani, bado tungekuwa naye, kila nikienda nyumbani, nilikuwa napata mtu wa kuzungumza naye. Sasa niko peke yangu, ninaishi na polisi. Sina mtu kutoka kwa familia yetu, sina chochote. Ni polisi tu. Ninaporudi nyumbani, natazama tu makaburi,” alisema.

Rigathi pia alizungumza kuhusu kaka ya mkewe, Pastor Dorcas ambaye pia ni mlevi.

Alisema kwamba kuna watu wengine wengi ambao wameathiriwa na ulevi lakini wanateseka kimya kimya.

"Tunapopigana na pombe hii, sio siasa. Tunazungumza huku tukiwa na uchungu mwingi moyoni kwa sababu tumeona jinsi pombe ilivyotuumiza sisi, majirani na marafiki zetu,” alisema.