Kamene Goro azungumzia madai ya ujauzito, aeleza sababu ya shida yake ya kutembea

Amebainisha kuwa upasuaji wa goti aliofanyiwa mapema mwaka huu uliathiri mtindo wake wa kutembea.

Muhtasari

•Kamene amepuuzilia mbali tetesi za ujauzito ambazo zimekuwa zikienezwa kwenye mitandao ya kijamii katika siku za hivi majuzi.

•Alizungumzia jinsi ambavyo amekuwa na safari ngumu ya kupona, akibainisha kuwa amekuwa akitembea kwa magongo kwa muda mrefu.

Kamene Goro/
Kamene Goro/
Image: HISANI

Aliyekuwa mtangazaji wa redio, Kamene Goro amepuuzilia mbali tetesi za ujauzito ambazo zimekuwa zikienezwa kwenye mitandao ya kijamii katika siku za hivi majuzi.

Katika taarifa yake ya  Jumapili, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 32 alibainisha kuwa kumekuwa na ripoti nyingi za ujauzito ambazo zimeibuka kutokana na mtindo wake wa kutembea.

Video ambazo zilichukuliwa wakati wa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa siku kadhaa zilizopita zikimuonyesha akihangaika kutembea zimekuwa chimbuko la uvumi huo.

"Katika wiki iliyopita nimeona maoni mengi, uvumi kuhusu jinsi nilivyokuwa nikitembea kwenye siku yangu ya kuzaliwa, na kila mara inarudi kwenye hitimisho lile lile la kizamani la kutojali kwamba mimi ni mjamzito. Jameni, nilisema sitawahi kujibu lakini ninahisi ninafaa kwa sababu maoni hayo hayana msingi na ni ujinga,” Kamene Goro alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Huku akieleza sababu ya shida lake la kutembea, mtangazaji huyo wa zamani wa redio alibainisha kuwa ni athari za upasuaji wa goti aliofanyiwa mapema mwaka huu.

Kamene alizungumzia jinsi ambavyo amekuwa na safari ngumu ya kupona, akibainisha kuwa amekuwa akitembea kwa magongo kwa muda mrefu.

"Kumbuka Januari nilifanyiwa upasuaji kwenye goti ambalo liliniweka hospitalini kwa siku 5. Sijatembea kwa muda mrefu, ni katika kuelekea siku yangu ya kuzaliwa ambapo nilianza kujaribu kutembea bila magongo yangu,” alisema.

Aliongeza, "Ni mchakato mgumu kujaribu kurejesha shughuli na nguvu ya misuli kwenye goti, ndiyo sababu ninatembea au kutembea kwa njia ya kuchekesha. Ni ahueni ngumu sana kwa uaminifu."

Kufuatia tetesi za ujauzito wa hivi majuzi, mke huyo wa Deejay Bonez sasa amewataka watumiaji wa mtandao kufanya uchunguzi wa kina  kila mara na kuuliza kabla ya kufanya hitimisho.