Sababu kwa nini mwimbaji Ringtone Apoko hajakuwa akionekana mtandaoni yafichuliwa

Mwimbaji wa nyimbo za Injili Ringtone Apoko amerejea hadharani baada ya kutoonekana kwa takriban miezi mitatu

Muhtasari

•Mwimbaji huyo wa kibao Tenda Wema aliambia YouTuber Trudy Kitui kuwa hakuwepo kwa sababu za kibinafsi

•Amesema ana matumaini kuwa mambo yatakuwa mazuri mwaka huu.

Ringtone azungumzia utajiri wake.
Ringtone azungumzia utajiri wake.
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji wa nyimbo za Injili Ringtone amerejea hadharani baada ya kutoonekana kwa takriban miezi mitatu. Mwimbaji huyo alionekana mtandaoni mara ya mwisho mnamo Desemba 2023.

Siku ya Ijumaa Aprili 5, alikuwa katika chuo akitoa hotuba za hamasa kwa wanafunzi. Pia alijitolea kumlipia karo mwanadada anayekwenda kusoma nchini Uingereza

“Mwaka huu nataka nifanye mambo kirahisi, watu huwa wananinyanyasa na nakaa kimya, nimejifunza ukiwa nayo watu wanakufurahia, ukikosa watu wanakucheka, katika maisha kuna kupanda na kushuka,” aliandika.

Mwimbaji huyo wa Tenda Wema aliambia YouTuber Trudy Kitui kuwa hakuwepo kwa sababu za kibinafsi

Alitaja changamoto ya pesa na akapuzilia mbali uvumi kuwa amekumbwa na msongo wa mawazo.

"Sina msongo wa mawazo. Labda nyinyi watu mnafikiria hivyo, labda kama nyinyi mlikuwa munaona ni depression labda ni nyinyi mnaona vibaya."

"Nimekuwa nikipata changamoto za kibinafsi, lakini nashukuru Mungu amenisaidia nimetoka kwa matatizo hayo. Kuna wakati nilikuwa nasali mpaka chakula nakula parachichi, breakfast, lunch, supper. Nilikua nalima hayo maparachichi na yalikuwa mengi sana, yalikuwa yakishuka kutoka kwenye miti."

Ana matumaini kuwa mambo yatakuwa mazuri mwaka huu.

"Watu hupitia changamoto labda ili kuzirejesha kwenye kusudi lao," akidokeza kwamba anaweza kuwa amepotoka kutoka kwa Injili.

"Pesa ilifanya nikasahau, nikaenda mambo mengine so nimerudi na nimesema charity inaanzia nyumbani. Kuanzia hapa nitafanya miradi mingi ya jamii."

Ana muziki mpya na pia anatafuta mwanamke wa kuoa mwaka ujao. Sifa zake? Awe Kienyeji, awe na umbo la kujikunja na asiwe mwanamke mwenye sauti ya juu.