Kajala avunja kimya baada ya bintiye Paula kufichua ni mjamzito, atamzalia mjukuu hivi karibuni

Huku akipokea habari hiyo njema, Kajala alisema yuko tayari kuwa bibi (nyanya) mzuri.

Muhtasari

•Kajala ameonekana kujawa na bashasha baada ya binti yake Paula Kajala kutangaza kuwa anatarajia mtoto wake wa kwanza.

•Shangazi yake Paula, Kate Masanja pia alielezea furaha yake ya kuwa bibi hivi karibuni. 

amezungumza baada ya kugundua atakuwa nyanya hivi karibuni
Kajala amezungumza baada ya kugundua atakuwa nyanya hivi karibuni
Image: INSTAGRAM

Muigizaji mkongwe wa filamu bongo Fridah Kajala Masanja ameonekana kujawa na bashasha baada ya binti yake Paula Kajala kutangaza kuwa anatarajia mtoto wake wa kwanza.

Paula na mpenzi wake Omary Mwanga almaarufu Marioo mnamo Alhamisi asubuhi walifichua kuwa hivi karibuni watakuwa wazazi wa mtoto wao wa kwanza pamoja.   

Wapenzi hao wawili walitoa tangazo lao zuri kwenye mtandao wa Instagram ambapo walionyesha ujauzito mzito wa Paula.

Huku akipokea habari hiyo njema, Kajala alisema yuko tayari kuwa bibi (nyanya) mzuri. 

 “Bibi (nyanya) nilie changamka hapa,” Kajala alijibu chini ya binti yake.  

 Shangazi yake Paula, Kate Masanja pia alielezea furaha yake ya kuwa bibi hivi karibuni. 

Huku akijibu chapisho la Marioo, Kajala alimtambua staa huyo wa bongo fleva kama mkwe wake.  

“Mkweee,” alisema na kuambatanisha maoni yake na emoji za moyo kuashiria mapenzi.

Alhamisi asubuhi, Marioo na Paula walitoa tangazo la kipekee la pamoja wakifichua kwamba wanatarajia mtoto wao wa kwanza pamoja.

Wawili hao walishiriki video nzuri iliyowaonyesha wakisoma gazeti lenye kichwa cha habari cha ‘A baby is on the way’ na pia kuonyesha tumbo la Paula lililochomoza.

“Ninatarajia mtoto na mpenzi wangu. Kuanzia mbili hadi tatu,” Paula aliandika chini ya video ambayo alichapisha kwenye Instagram.

Katika video hiyo, mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 22 alionekana akiwa na ujauzito mkubwa huku yeye na mpenzi wake wakionyesha picha za kijusi kinachokua tumboni mwake.

Marioo ambaye kwa jina halisi ni Omary Mwanga pia alishiriki furaha yake ya kuwa baba hivi karibuni na akamshukuru binti wa muigizaji Kajala Masaja kwa kubeba ujauzito wake.

"Kuongeza memba mpya kwenye kikosi chetu! Soon inshallah.. Najivunia wewe malkia @therealpaulahkajala Mungu akubariki wewe na familia,” Marioo alisema.

Kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja sasa, Paula na msanii Marioo wamekuwa katika kile kinachotajwa kuwa mapenzi mazito, huku Kajala tarari akionekana kukubali penzi lao na kumtaja waziwazi Marioo kama mkaza mwana wake.