Paula ampongeza babake anapoadhimisha miaka 10 ya ndoa na aliyechukua nafasi ya mamake

Haya yanajiri siku chache tu baada ya muigizaji Kajala Masanja kumuomba msamaha mzazi mwenzake, P-Funk Majani.

Muhtasari

•Bw Majani ambaye anasifiwa kwa mchango wake mkubwa katika kuanzisha muziki wa Bongoflava aliadhimisha miaka kumi ya harusi na mkewe Samira.

•“Heri ya kumbukumbu ya ndoa ya  miaka,” Paula aliandika na kuambatanisha maoni yake kwa emoji za upendo.

P-funk Majani, Marioo, Paula, Kajala, na Samira
Image: INSTAGRAM// P-FUNK MAJANI

Mwanamitindo maarufu wa Tanzania Paul Paul alimpongeza baba yake Paul Matthysse almaarufu P-Funk Majani wakati akiadhimisha hatua muhimu katika ndoa yake.

Siku ya Ijumaa, Bw Majani ambaye anasifiwa kwa mchango wake mkubwa katika kuanzisha muziki wa Bongoflava aliadhimisha miaka kumi ya harusi na mkewe Samira.

Wakati akisherehekea muongo mmoja wa ndoa yake, producer huyo kutoka Tanzania alichapisha picha nzuri akiwa na mkewe na kuandika;

"Heri ya kumbukumbu ya miaka 10 ya harusi kwetu,"

Mamia ya watumiaji wa Instagram akiwemo binti yake Paula waliwasherehekea kwa mafanikio hayo.

“Heri ya kumbukumbu ya ndoa ya  miaka,” Paula aliandika na kuambatanisha maoni yake kwa emoji za upendo.

Katika majibu yake, Bw Majani aliandika, “Asante.”

Haya yanajiri siku chache tu baada ya wawili hao kukutana katika hafla ya baby shower iliyoandaliwa mapema wiki hii kusherehekea ujauzito wa Paula.

Wakati wa hafla hiyo, mwigizaji wa filamu bongo Fridah Kajala, ambaye ni mama mzazi wa Paula aliomba msamaha kwa baba huyo ya binti yake.  

Akizungumza, mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize alikiri kwamba amemkosea baba ya binti yake mara kwa mara na anajutia hilo.

Alithibitisha hawajakuwa katika maelewano mazuri kwa muda na kuwa walikuwa wamepigana block kila mahali mitandaoni na kwenye simu.

“Kuna vitu vingi sana ambavyo vilikuwa vinaendelea na hakuwa anavipenda kama baba, na mimi nilikuwa najua kabisa kuna vitu nilikuwa navikosea, kwa hiyo ilinibidi kuomba radhi kama mama, ilmradi kila kitu kiwe sawa kwa binti yetu,” Kajala alisema.

 Aidha, kando na kuomba msamaha kwa mzazi mwenziwe, Kajala alimhongera mke mpya wa aliyekuwa mumewe kwa kuwa daraja ya mapatano baina yake na P-Funk.

“Kuna vitu nilikuwa nikivizingua yeye anakasirika na Paula anajua kabisa hapa baba amekasirika kwa hiyo anaamua kumtafuta, lakini sisi kimbilio letu lilikuwa ni Samira, mke wa P-Funk, wako miaka mingi na wana watoto 3.”

“Sisi tunampenda kwa sababu, mimi na Paul [P-Funk Majani] tumeblockiana kila mahali kwa ufupi, huwa hatuongei. Lakini nikiona kuna kitu kimefikia shingoni tunahitaji msaada kwa ajili ya Paula nitamfuata Samira na kumuelezea na yeye atafikisha ujumbe na kila kitu kitakuwa sawa,” Kajala alimmiminia sifa mkewe baba bintiye.

Kajala akimalizia alimsifia P-Funk Majani na kusema kwamba yeye ni baba mwema kwa bintiye huku akimkumbatia na kumtaka kumsamehe kwa sekeseke zote ambazo zimetokea baina yao siku za nyuma.

“Tunashukuru kwa uwepo wao, na Paul, nisamehe kama nimekukosea kwa vitu vyovyote, na wewe ni baba mwema na nakupenda,” Kajala alisema na kumkumbatia.