Marioo apokea upendo tele na baraka kutoka kwa mamake na babake Paula kufuatia ujauzito

Mwimbaji huyo alitoa shukurani zake kwa Kajala na mzazi mwenzake P-Funk Majani ambao aliwatambua kuwa ni wakwe zake.

Muhtasari

•Wakati akijibu ujumbe wa shukrani wa mwimbaji huyo, mamake Paula alimhakikishia mkwe wake wa mapenzi kwake.

•Bw Majani pia alimjibu staaa huyo wa bongo fleva na kumhakikishia kuwa kila kitu kiko sawa.

P-Funk Majani, Paula Kajala, Marioo, Kajala Masanja na mkewe P-Funk Majani
Image: INSTAGRAM// MARIOO

Staa wa Bongo, Omary Mwanga almaarufu Marioo aliwashukuru sana wazazi wa mpenzi wake Paula Kajala kufuatia karamu ya Baby Shower iliyofanyika wiki iliyopita.

Mwimbaji huyo wa kibao cha ‘Mi Amor’ aliingia katika ukurasa wake wa Instagram kutoa shukurani zake kwa muigizaji wa filamu bongo Fridah Kajala Masanja na mzazi mwenzake P-Funk Majani ambao aliwatambua kuwa ni wakwe zake.

"Hakuna Matata. Asanteni Baba na Mama Mkwe @majani187 & kajalafrida,” Marioo aliandika baada ya hafla ya Baby Shower iliyofanyika Ijumaa jioni.

Msanii huyo aliambatanisha ujumbe wake na picha zake, Paula, Kajala na Bw Majani ambazo zilichukuliwa wakati wa hafla hiyo ya kupendeza iliyoandaliwa kusherehekea ujauzito.

Muigizaji Kajala na mzazi huyo mwenzake ambaye aliachana naye takriban miongo miwili iliyopita walikuwa miongoni mwa wageni waliopamba hafla ya Marioo na Paula.

Wakati akijibu ujumbe wa shukrani wa mwimbaji huyo, mamake Paula alimhakikishia mkwe wake wa mapenzi kwake.

“Tunakupenda,” aliandika.

Bw Majani pia alimjibu staaa huyo wa bongo fleva na kumhakikishia kuwa kila kitu kiko sawa.

"Karibu, hakuna matata mwana," alisema.

Wakati wa hafla ya Ijumaa, mamake Paula alichukua fursa kuomba msamaha kwa baba ya binti yake.  

Akizungumza, mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize alikiri kwamba amemkosea Bw Majani mara kwa mara na anajutia hilo.

Alithibitisha hawajakuwa katika maelewano mazuri kwa muda na kuwa walikuwa wamepigana block kila mahali mitandaoni na kwenye simu.

“Kuna vitu vingi sana ambavyo vilikuwa vinaendelea na hakuwa anavipenda kama baba, na mimi nilikuwa najua kabisa kuna vitu nilikuwa navikosea, kwa hiyo ilinibidi kuomba radhi kama mama, ilmradi kila kitu kiwe sawa kwa binti yetu,” Kajala alisema.

 Aidha, kando na kuomba msamaha kwa mzazi mwenziwe, Kajala alimhongera mke mpya wa aliyekuwa mumewe kwa kuwa daraja ya mapatano baina yake na P-Funk.

“Kuna vitu nilikuwa nikivizingua yeye anakasirika na Paula anajua kabisa hapa baba amekasirika kwa hiyo anaamua kumtafuta, lakini sisi kimbilio letu lilikuwa ni Samira, mke wa P-Funk, wako miaka mingi na wana watoto 3.”

“Sisi tunampenda kwa sababu, mimi na Paul [P-Funk Majani] tumeblockiana kila mahali kwa ufupi, huwa hatuongei. Lakini nikiona kuna kitu kimefikia shingoni tunahitaji msaada kwa ajili ya Paula nitamfuata Samira na kumuelezea na yeye atafikisha ujumbe na kila kitu kitakuwa sawa,” Kajala alimmiminia sifa mkewe baba bintiye.

Kajala akimalizia alimsifia P-Funk Majani na kusema kwamba yeye ni baba mwema kwa bintiye huku akimkumbatia na kumtaka kumsamehe kwa sekeseke zote ambazo zimetokea baina yao siku za nyuma.

“Tunashukuru kwa uwepo wao, na Paul, nisamehe kama nimekukosea kwa vitu vyovyote, na wewe ni baba mwema na nakupenda,” Kajala alisema na kumkumbatia.