Drama huku Zuchu akihusika kwenye makabiliano makali na Harmonize na mpenziwe Poshy Queen

Haya yanajiri katika kipindi ambacho Zuchu na Diamond wameripotiwa kuachana tena.

Muhtasari

•Drama ilianza baada ya Konde Boy kumkejeli Zuchu muda mfupi baada ya kutoa taarifa kueleza kwa nini alijiondoa kwenye uhusiano wake na Diamond .

•“Sisi koma. Mwili mzima kucha hadi nywele kalio la kushoto!! Muulize tena!! Shem kama shem nimeongiaje humu,” Poshy Queen aliandika.

Zuchu, Harmonize, Poshy Queen
Image: HISANI

Ulimwengu wa bongo mnamo siku ya Jumanne ulipamba moto huku malkia wa WCB Zuhura Othman almaarufu Zuchu na mpenzi wa Harmonize Poshy Queen wakirushiana cheche za maneno makali  kwenye mitandao ya kijamii.

Drama ilianza baada ya Konde Boy kumkejeli Zuchu muda mfupi baada ya kutoa taarifa kueleza kwa nini alijiondoa kwenye uhusiano wake na Diamond Platnumz.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide alichapisha video ambayo ilionekana kumshambulia moja kwa moja Zuchu na alionekana kumcheka kutokana na matatizo katika uhusiano wake.

 

“Kibonge koma, @harmonize_tz Huna hit mjini una kazi ya kuchambana tu mxiew haujui nini sijui eeh nioneshe,” Zuchu alimwandikia Harmonize kupitia mtandao wa Instagram.

Aliongeza, “Harmonize baba zima kazi ya kudandia visivyokuhusu. Mwanamke wako yuko busy kuomba nafasi kwa huyo unayejifanya nusu yako shenzi. Koma kistuli.”

Kufuatia kushambuliwa kwa mpenzi wake, Poshy Queen alizamia kwenye akaunti yake ya Instagram na kumshambulia Zuchu akimkejeli kuhusu mwili wake mdogo.

“Sisi koma. Mwili mzima kucha hadi nywele kalio la kushoto!! Muulize tena!! Shem kama shem nimeongiaje humu,” Poshy Queen aliandika.

Harmonize naye alionekana kuendelea kumkejeli Zuchu kwenye akaunti yake ya Instagram kupitia video za kejeli na kauli ambazo alishare.

Haya yanajiri katika kipindi ambacho Zuchu na Diamond wameripotiwa kuachana tena.

Kulikuwa na tetesi kuwa binti huyo wa malkia wa taarab Khadija Kopa amemuacha Simba, ambaye pia ni bosi wake baada ya kumtambulisha ex wake Sarah katika tamasha la muziki la hivi majuzi nchini Tanzania. Wakati wa tamasha hilo, Diamond alimwita Sarah jukwaani na kufunguka jinsi alivyomshawishi kuandika wimbo wa ‘Kamwambie.’

Zuchu hata hivyo alikanusha madai ya kuachana na bosi huyo wa WCB kwa sababu ya Sarah na badala yake akaeleza kuwa mpenzi wake ndiye aliyemfanya akosewe heshima na watu.