"Anacheza na kifo!" Harmonize atuma onyo kali kwa Zari baada ya mumewe kutaka kupigana naye

“Zari unalijua hili?? Mtu wako anajaribu kucheza na kifo!" Harmonize alimwandikia Zari.

Muhtasari

•Kulingana na Bw Lutaaya, mchuano na Konde Boy ingeweza kuwaingizia mapato mengi na pia kusaidia kupata pesa nyingi za kutoa misaada.

•Konde Boy alitoa onyo kwa mfanyabiashara huyo akimshauri kwamba huenda akataka kubadili mawazo yake.

ametuma onyo baada ya mumewe Zari kuomba kupigana naye.
Harmonize ametuma onyo baada ya mumewe Zari kuomba kupigana naye.
Image: HISANI

Bosi wa lebo ya Konde Music Wordwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize alikuwa na ujumbe maalum kwa mwanasosholaiti wa Uganda, Zari Hassan baada ya mume wake Shakib Cham Lutaaya kuomba washiriki naye pambano la ndondi nchini Tanzania.

Siku ya Alhamisi, staa huyo wa bongo fleva alidokeza kuhusu kujiondoa kwenye tasnia ya muziki na kuangazia ndondi kama taaluma yake mpya.

Kupitia katika Instastori zake, alisema kuwa amejikita katika mazoezi ili ashiriki mchuano wa ngumi na bondia Hassan Mwakinyo, akisema kuwa tasnia ya muziki ina chuki nyingi sana.

“Acha nizingatie katika kumchapa ngumi Mwakinyo ili nibadilishe taaluma. Chuki ni nyingi sana huku [kwenye muziki]. Pengine kutakuwa na amani, najua nitafaulu, Mungu nisaidie,” Harmonize alisema

Mfanyabiashara wa Uganda Shakib Lutaaya, ambaye ni mume wa mzazi mwenza wa Diamond Platnumz, Zari Hassan ni miongoni mwa watu waliomwandikia mtunzi huyo wa kibao ‘Single Again’ kumpongeza na pia kuomba pambano la ngumi.

Kulingana na Bw Lutaaya, mchuano na Konde Boy ingeweza kuwaingizia mapato mengi na pia kusaidia kupata pesa nyingi za kutoa misaada.

“Habari za siku rafiki, pongezi kwenye hatua hii mpya ya ndondi, ningependa kuwa na mchezo wa ndondi na wewe pia Tanzania. Tungepata pesa kutoka kwayo na kufanya hisani pia. Natarajia kusikia kutoka kwako hivi karibuni kwenye hili #ShakibCham,” Shakib alimwandikia Harmonize katika gumzo ambalo mwimbaji huyo wa bongo fleva alifichua kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Katika jibu lake, Konde Boy alitoa onyo kwa mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 32 akimshauri kwamba huenda akataka kubadili mawazo yake.

“LOL. Tazama hii kwanza inaweza kukufanya ubadili mawazo,” Harmonize alimwandikia Shakib.

Konde Boy aliendelea kuhoji iwapo Zari alikuwa anafahamu ujumbe wa mumewe kwake akionya kuwa ana uwezo wa kumdhuru.

“Zari unalijua hili?? Mtu wako anajaribu kucheza na kifo!" Harmonize alimwandikia Zari.

Katika sasisho lingine siku ya Ijumaa, staa huyo wa bongo fleva alibainisha kuwa hataachana na muziki kwa ajili ya ndondi kama alivyotangaza awali.

Alisema kuwa ataendelea kupigana katika tasnia ya muziki kwani wanawake wanahitaji mtu kama yeye wa kuwatetea na kuwasifia kwa nyimbo.