"Nakupenda hata nisipokuwepo" Bahati amwambia bintiye na ex wake Yvette Obura

Bahati amesherehekea mtoto wake wa kwanza Mueni ambaye alimpata kutokana na uhusiano wake wa awali.

Muhtasari

•Bahati alimhakikishia msichana huyo wa miaka minane kuhusu upendo wake mkubwa kwake hata ingawa hawako pamoja kila mara.

•Bahati alisindikiza ujumbe wake na picha nzuri ya kumbukumbu yake na mtoto huyo wake wa kwanza iwakiwa wamelala kwenye nyasi.

amemhakikishia bintiye Mueni Bahati kuhusu upendo wake kwake.
Bahati amemhakikishia bintiye Mueni Bahati kuhusu upendo wake kwake.
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji wa nyimbo za mapenzi Kelvin Kioko almaarufu Bahati amesherehekea mtoto wake wa kwanza Mueni Bahati ambaye alimpata kutokana na uhusiano wake wa awali.

Katika chapisho la Jumamosi, baba huyo wa watoto wanne alimhakikishia msichana huyo wa miaka minane kuhusu upendo wake mkubwa kwake hata ingawa hawako pamoja kila mara.

Mueni ni bintiye Bahati na mpenzi wake wa zamani Yvette Obura.

"Nakupenda hata nisipokuwepo," Bahati alimwandikia binti yake kwenye mtandao wa Instagram na kuambatanisha ujumne wake na emoji ya moyo kuashiria upendo.

Mwimabji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alisindikiza ujumbe wake na picha nzuri ya kumbukumbu yake na mtoto huyo wake wa kwanza iwakiwa wamelala kwenye nyasi.

Licha ya wazazi wake kuachana miaka mingi iliyopita na kutoishi tena pamoja, Mueni anaonekana kuwa bado sehemu muhimu ya familia ya Bahati. Mara nyingi anaonekana nyumbani kwa Bahati na hata hushiriki muda na watoto wengine wa mwimbaji huyo pamoja na mke wake wa sasa Diana Marua.

Katikati mwa mwaka jana, Mueni aliwasisimua wanamitandao kufuatia ujumbe wake mzuri kwa babake mnamo siku ya kuwasherehekea akina baba duniani.

Katika video hiyo iliyochapishwa na Bahati kwenye mtandao wa Instagram, Mueni alimsifu mwimbaji huyo kwa kuwa baba mzuri.

Mrembo huyo mwenye umri wa miaka nane aliangazia baadhi ya mambo mazuri ambayo mzazi huyo wake amemfanyia yeye na ndugu zake wengine ikiwa ni pamoja na kuwanunulia nguo, kuwapa makazi mazuri na elimu.

“Kheri ya siku ya akina baba, asante kwa kutununulia nyumba nzuri, asante kwa kutupeleka shule nzuri ambayo walimu hawatupigi, asante kwa kunisaidia kuwa na afya njema na pia kuninunulia nguo, na asante kwa kuwa mwaminifu kwetu," Mueni alimwambia babake kwa kujiamini.

Malkia huyo mdogo alitangulia kumhakikishia Bahati kuhusu upendo wao mkubwa kwake kwa ujumbe wa kipekee ambao ulionekana kumwacha mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili katika hali ya mshtuko.

"Hata ukifa utajua tu kwamba tunakupenda," Mueni alisema.

Bahati ambaye alionekana kuingizwa wasiwasi na ujumbe huo alisema, "Lakini sifi, asante lakini mimi sifi."

Mueni aliendelea kumweleza baba yake kwamba anapoendelea kuzeeka kuna uwezekano mkubwa wa yeye kufa.

"Ukizeeka, utakufa pia," alisisitiza.

Bahati aliucheka tu ujumbe wa kipekee wa binti huyo wake wa kwanza na alikuwa na shauku ya kujua ni wapi alijifunza hotuba hiyo.

Mueni kwa unyenyekevu alifichua kuwa mwana wa kulea wa Bahati, Morgan Bahati ndiye aliyemfundisha.

Mueni ni mtoto wa kwanza wa Bahati  na Yvette ambaye alizaliwa takriban miaka minane iliyopita kabla ya wazazi wake kutengana.

Licha ya kutengana na Yvette miaka mingi iliyopita, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili ameendelea kushirikiana naye vizuri katika malezi. 

Mke wa Bahati, Diana Marua pia anaonekana kumkubali binti huyo wa kwanza wa mwimbaji huyo na pia anamsaidia katika malezi. Hata hivyo kumekuwa na madai ya ugomvi usiyojulikana kati ya Diana na Yvette.