Harmonize? Kajala atupa vijembe kwa wapenzi wa zamani

Alidai kuwa ni wale tu ambao mtu ana watoto nao wanaoweza kutajwa kuwa ni wapenzi wa zamani.

Muhtasari

•Kajala alichapisha picha ya nukuu kuhusu wapenzi wa zamani kutoka kwa mwanahabari wa Wasafi Media, Oscar Oscar.

•Mwimbaji Harmonize ndiye mpenzi wa zamani wa muigizaji huyo mkongwe wa filamu bongo anayefahamika zaidi.

Image: HISANI

Muigizaji maarufu wa Tanzania Fridah Kajala Masanja ameonekana kuwatupia vijembe wapenzi wake wa zamani.

Siku ya Jumanne, mama huyo wa binti mmoja alichapisha picha ya nukuu kuhusu wapenzi wa zamani kutoka kwa mwanahabari wa Wasafi Media, Oscar Oscar.

Katika nukuu hiyo, mwanahabari Oscar alidai kuwa ni wale tu ambao mtu ana watoto nao wanaoweza kutajwa kuwa ni wapenzi wa zamani.

“Ex ni mtu uliyezaa naye mtoto. Hao wengine ni watu tu mnaojuana,” nukuu iliyoshirikiwa na Kajala ilisomeka.

Kwa kuposti chapisho la Oscar, mpenzi huyo wa zamani wa mwimbaji Harmonize alionekana kukubaliana na maoni ya mwandishi huyo wa habari.

Bosi wa Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ndiye mpenzi wa zamani wa muigizaji huyo mkongwe wa filamu bongo anayefahamika zaidi.

Malkia huyo mwenye umri wa miaka 40 kwa upande mwingine ana binti wa miaka 21 ambaye alimpata na mtayarishaji muziki mkongwe wa Tanzania P-Funk Majani.

Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Mwezi uliopita, wazazi wenza hao wawili walikutana katika hafla ya baby shower iliyoandaliwa kusherehekea ujauzito wa binti yao Paula Paul.

Wakati wa hafla hiyo, mwigizaji wa filamu bongo Fridah Kajala, ambaye ni mama mzazi wa Paula aliomba msamaha kwa baba huyo ya binti yake.  

Akizungumza, mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize alikiri kwamba amemkosea baba ya binti yake mara kwa mara na anajutia hilo.

Alithibitisha hawajakuwa katika maelewano mazuri kwa muda na kuwa walikuwa wamepigana block kila mahali mitandaoni na kwenye simu.

“Kuna vitu vingi sana ambavyo vilikuwa vinaendelea na hakuwa anavipenda kama baba, na mimi nilikuwa najua kabisa kuna vitu nilikuwa navikosea, kwa hiyo ilinibidi kuomba radhi kama mama, ilmradi kila kitu kiwe sawa kwa binti yetu,” Kajala alisema.

 Aidha, kando na kuomba msamaha kwa mzazi mwenziwe, Kajala alimhongera mke mpya wa aliyekuwa mumewe kwa kuwa daraja ya mapatano baina yake na P-Funk.

“Kuna vitu nilikuwa nikivizingua yeye anakasirika na Paula anajua kabisa hapa baba amekasirika kwa hiyo anaamua kumtafuta, lakini sisi kimbilio letu lilikuwa ni Samira, mke wa P-Funk, wako miaka mingi na wana watoto 3.”

“Sisi tunampenda kwa sababu, mimi na Paul [P-Funk Majani] tumeblockiana kila mahali kwa ufupi, huwa hatuongei. Lakini nikiona kuna kitu kimefikia shingoni tunahitaji msaada kwa ajili ya Paula nitamfuata Samira na kumuelezea na yeye atafikisha ujumbe na kila kitu kitakuwa sawa,” Kajala alimmiminia sifa mkewe baba bintiye.

Kajala akimalizia alimsifia P-Funk Majani na kusema kwamba yeye ni baba mwema kwa bintiye huku akimkumbatia na kumtaka kumsamehe kwa sekeseke zote ambazo zimetokea baina yao siku za nyuma.

“Tunashukuru kwa uwepo wao, na Paul, nisamehe kama nimekukosea kwa vitu vyovyote, na wewe ni baba mwema na nakupenda,” Kajala alisema na kumkumbatia.