Wakati wa hisia kwa Bahati na Diana Marua huku mtoto wao wa kulea, Morgan akiwaaga

Diana Marua alidhihirisha upendo wake mkubwa kwa kijana huyo na kumtaka aende akawafanye wajivunie.

Muhtasari

•Bahati amefichua huwa ni wakati wa kihisia kwao wakati kijana huyo anapokuwa akiondoka nyumbani kurejea shuleni.

•Bahati alizungumzia jinsi anavyojivunia maendeleo ya mvulana huyo wa miaka 13 shuleni na jinsi wanavyomlea vizuri.

 

Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwimbaji wa nyimbo za mapenzi Kelvin Bahati aliandika taarifa ya kihisia siku ya Jumatano baada ya yeye na mkewe Diana Marua kumsindikiza mtoto wao wa kulea Morgan Bahati kurudi shuleni.

Morgan ambaye amekuwa akiishi na familia ya Bahati kwa takriban muongo mmoja alijiunga na shule ya bweni mapema mwaka huu na mwimbaji huyo amefichua kwamba huwa ni wakati wa kihisia kwao wakati kijana huyo anapokuwa akiondoka nyumbani kurejea shuleni.

"Zaidi ya miaka 10 sasa, mwana wetu @morgan_bahati hajawahi kuwa mbali nasi na kila mara anapoondoka kwenda shule ya bweni huwa ni wakati wa hisia kwetu," Bahati alisema katika taarifa aliyoichapisha kwenye mtandao wa Instagram Jumatano.

Aliambatanisha taarifa hiyo na picha zilizomuonyesha yeye, mkewe Diana na mtoto wao Morgan wakiwa wamekaa ndani ya gari lao wakielekea shuleni.

Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili aliendelea kuzungumzia jinsi anavyojivunia maendeleo ya mvulana huyo wa miaka 13 shuleni na jinsi wanavyomlea vizuri.

"Tunafurahi kumuona akiingiana na maisha mapya ya shule na ni dhihirisho kwamba tunamlea mtu hodari, bingwa aliye tayari kushinda changamoto hapa sokoni," alisema.

“Mwana wetu, nenda ukafanikiwe kwa jina la Yesu,” aliongeza.

Kwa upande wake, Diana Marua alidhihirisha upendo wake mkubwa kwa kijana huyo na kumtaka aende akawape fahari shuleni.

“Nakupenda mtoto wangu @morgan_bahati. Inatufanya tujivunie,” Diana alisema.

Bahati alimchukua Morgan kuwa mtoto wake mwaka wa 2014 wakati alipoenda kutumbuiza katika nyumba ya  watoto yatima ya ABC ambapo alikulia pia baada ya mama yake kuaga dunia.

Baada ya Bahati kutumbuiza, mvulana huyo alikataa kurejea katika kituo hicho cha watoto na akataka kwenda naye.

Huku akizungumzia matukio ya kipindi hicho miaka miwili iliyopita, msanii huyo alisema alikuwa wakati huo hakuwa na uwezo mkubwa wa kifedha kumwezesha kuasili mtoto.

“Baada ya shoo mtoto  mdogoMorgan mwenye umri wa miaka 2 alilia kwenda na mimi nyumbani, ilikuwa ngumu kwangu kwa sababu nilikuwa bado natatizika kifedha.. Mbaya zaidi niliishi kwenye chumba kidogo na sikuwa na mtu wa kumlea mtoto kwa sababu nilkuwa nikiikaa peke yangu,'' alisema.

Morgan amekuwa akiishi na Bahati tangu wakati huo na mwimbaji huyo amekuwa akimtunza vizuri kama mtoto wake wa kuzaa.