Waimbaji wa kikundi cha Zabron singers, kupitia mwimbaji wao mkuu Japhet Zabron wamezima uvumi kuwa walihusika katika ajali ya barabarani.
Akizungumza na Wasafi TV, Japhet alifunguka;
"Watu wanatuua tukiwa hai. Nilikutana na watu kijijini kwetu wakisema walidhani tayari tumeaga dunia," alisema.
Aliendelea "Pia kumekuwa na habari kwenye mitandao ya kijamii kwamba tulipata ajali. Tulipata maswali mengi kutoka kwa mashabiki wetu wakituuliza nini kinaendelea."
"Nataka kuwaambia mashabiki wetu kwamba tuko hai, hakuna hata mmoja kati ya wanachama wetu aliyepata ajali. Tunamshukuru Mungu."
Japhet alisema ni mwezi mmoja sasa tangu waanze kusikia watu wakizungumzia ajali hiyo feki.
Waimbaji wa Zabron waliibuka kidedea kupitia wimbo wao wa 'Mkono Wa Bwana.' Tangu wakati huo, wamewafurahisha mashabiki kwa nyimbo nyingine nyingi miongoni mwao 'Uko Single' 'Sweetie Sweetie' 'Sisi Ndio Wale' miongoni mwa zingine.
Wanakikundi wengine ni pamoja na Victoria Zabron, Jamila Dotto, Samuel Joseph, Semroza Godfrey, Mark Bukuru, Grace Madata na Joyce Zabron.