Mwanasosholaiti maarufu wa Uganda Zari Hassan ameweka wazi kuwa ana furaha na ametosheka kuishi mbali na mume wake Shakib Cham Lutaaya.
Hivi majuzi, wanandoa hao walifanya mazungumzo ya wazi ambapo walizungumzia uhusiano wao wa umbali mrefu na jinsi wameweza kudumisha ndoa yao licha ya kutoishi pamoja.
Zari alisema kwamba mwanzoni, mara tu baada ya ndoa yao, hakuwa na uhakika kuhusu jinsi ndoa yao ingefanya kazi wakati wakiishi katika nchi tofauti.
“Nilishangaa, tutaishi aje sehemu tofauti wakati tumeoana. Lakini nadhani inafanya kazi,” Zari alisema kwenye video iliyochapishwa kwenye YouTube.
Shakib alifichua kuwa baada ya ndoa yao, alikuwa tayari kuhamisha biashara zake kutoka Uganda hadi Afrika Kusini ili kuishi na mkewe.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 32 alisema alikuwa amepima kila kitu na kuamua kuhamia Afrika Kusini kabla ya baadaye kubadili uamuzi wake.
“Niligundua jambo hili la tuko pamoja, ninakuja na kukuona, inahisi kama mpya kabisa. Niliona kama ina maana na nikagundua kwamba ikiwa tutaendesha mapenzi yetu hivi, tunaweza kwenda hadi miaka 40,” alisema.
Zari alibainisha kwamba hangetaka hata mume wake aishi naye Afrika Kusini.
Alikiri kwamba hataki kuwa na mumewe huyo mwenye umri wa miaka 32 kila siku kwa kuwa inaweza kumchosha.
“Hapana, ningechoka. Siwezi kukuvumilia kwa mwezi. Ni nyingi sana, niko bize sana. Kufanya matangazo mengi, ninasafari, kuna Watoto, biashara, kisha mimi na maisha yangu ya kijamii na kwa mimi kuweka hayo pamoja yote na kukuongeza sasa wewe kama mume wangu, ukweli kwamba hatuko kwenye kila mmoja kwa masaa 24 inachosha,” Zari alisema.
Wakizungumza wakati wa kipindi hicho cha mazungumzo, wawili hao walifichua kuwa sababu kuu ya kutoishi pamoja ni kwa sababu wana kazi ya kuendesha.
“Unaishi Afrika Kusini, mimi naishi Uganda. Lakini ninaweza kukuona wakati wowote ninapotaka kukuona. Unaweza kuja hadi Uganda wakati wowote unapotaka kuniona, nadhani ni jambo zuri,” Shakib alisema kwenye mazungumzo hayo.
Aliongeza, "Sio jambo baya kwa watu ambao wana shughuli nyingi kila wakati. Kumbuka nina kazi Uganda na wewe una kazi yako mwenyewe huko Afrika Kusini, na hakuna jinsi utaacha kazi yako na kuhamia hapa (Uganda) kwa kudumu.
Na hakuna njia nitahamia Afrika Kusini kabisa na kuacha kazi yangu. Nadhani ukweli kwamba tunaweza kumudu ndege hadi Afrika Kusini, na wewe kuruka hadi Uganda, inafanya kuwa sawa."