Mulamwah afichua zaidi kuhusu binti yake mzaliwa wa kwanza, kwa nini huwa hamposti

Alifichua kuwa mzazi mwenzake alifariki kabla ya yeye kukutana na ex wake mwingine, Carrol Sonie.

Muhtasari

•“Baada ya kumpoteza mama yake, alikaa na shangazi zake kwa muda mrefu zaidi. Nimekuwa nikisapoti, nimekuwepo," Mulamwah alisema.

•Aliweka wazi kuwa hana nia ya kum’posti bintiye kwani hatua hiyo inaweza kuingilia usiri wake na watu wengine wa karibu.

Mulamwah
Mulamwah
Image: HISANI

Mchekeshaji na mtayarishaji wa maudhui wa Kenya David Oyando almaarufu Mulamwah ametoa maelezo zaidi kuhusu mtoto wake wa kwanza ambaye alitambulisha hivi majuzi.

Siku ya Jumatano, msanii huyo mwenye umri wa miaka 31 aliwashangaza wanamitandao kwa kufichua kuwa ana binti wa miaka saba, ambaye alipata na mpenzi wake wa zamani ambaye aliaga dunia.

Akiongea kwenye video iliyochapishwa kwenye chaneli ya YouTube ya Ruth K’, Mulamwah alifichua kuwa bintiye alichukuliwa na shangazi zake mamake alipofariki.

“Baada ya kumpoteza mama yake, alikaa na shangazi zake kwa muda mrefu zaidi. Nimekuwa nikisapoti, nimekuwepo. Tumekuwa tukikutana. Bestie anamjua, huwa anakuja hapa Nairobi tunakaa na yeye. Wakati mwingine anakuwa hapa kwa nyumba,” Mulamwah alieleza.

Alifichua kuwa bintiye sasa ana umri wa miaka sita, karibu kutimiza miaka saba.

Mchekeshaji huyo hata hivyo aliweka wazi kuwa hana nia ya kum’posti bintiye kwani hatua hiyo inaweza kuingilia usiri wake na watu wengine wa karibu.

"Yeye ni mzuri sana. Hatujataka kumpost kwa sababu maisha yake iko private hivyo. Sio lazima utangaze kila kitu. Ukisema, tena huko shule yake ataanza kuwa na mashida, walimu wake wataanza kuwa na maneno na yeye. Shangazi wake wataanza kwenye umma,” alisema.

Mtayarishaji wa maudhui huyo alizungumza hayo wakati akimtetea nyanyake kwa kusema ana wajukuu wa kiume pekee.

Katika video hiyo, Mulamwah pia alifichua kuwa mzazi mwenzake alifariki kabla ya kukutana na mpenzi wake mwingine wa zamani, Carrol Sonie.

Siku ya Jumatano jioni, Mulamwah alifichua kuwa ana binti wa miaka saba anayeitwa Lisa.

Hata hivyo, zaidi alifichua habari za kusikitisha kwamba mama ya bintiye alifariki kipindi kilichopita.

"Binti yangu mzaliwa wa kwanza, Lisa, mwenye umri wa miaka 7, akielekea miaka 8, tulimpoteza mama yake wakati fulani, lakini ni sawa," Mulamwah alisema kupitia Instagram.

Mulamwah aliendelea kueleza kuwa kuna mambo mengi kuhusu maisha yake ambayo watu hawayajui, ambayo baadhi yake atakuwa akiyaweka wazi hivi karibuni ili kuweka mambo wazi na kujibu maswali ambayo watu wanaweza kuwa nayo.

Pia alimhakikishia binti yake kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

"Upendo mwingi," aliandika chini ya picha ya kumbukumbu yake na Lisa.

Ufichuzi huo mpya uliwashangaza wengi kwani siku zote watu wamekuwa wakiamini kuwa mchekeshaji huyo ana watoto wawili pekee, mmoja wa kike ambaye alipata na aliyekuwa mpenzi wake Carrol Sonie na mwingine wa kiume aliyepata na mpenzi wake wa sasa Ruth K.