"Mama alidanganya!" Tiffah apigwa na butwaa baada ya Diamond kumfanyia surprise ya kupendeza

“Nilidhani hutakuja. Mama alisema hautakuja. Mama alidanganya,” Tiffah alisema kwa mshtuko.

Muhtasari

•Diamond alim’surprise bintiye Latiffah kwa kujitokeza kwenye sherehe ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa bila yeye kujua.

•Tiffah alionekana kupigwa na butwaa akimkaribisha babake kwenye tafrija hiyo ya kifahari iliyohudhuriwa na familia na marafiki.

wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Tiffah
Diamond na Tiffah wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Tiffah
Image: HISANI

Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz alim’surprise bintiye Latiffah Dangote kwa kujitokeza kwenye sherehe ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa bila yeye kujua.

Diamond aliwasili nchini Afrika Kusini siku ya Jumamosi, akiwa ameandamana na timu yake na wakaenda mpaka mahali palipokuwa pakifanyika sherehe ya bintiye. Baada ya kuwasili, alibainisha kuwa alikuwa na nia ya kum’surprise mtoto huyo wake wa kwanza kwani hakuwa na taarifa kwamba angehudhuria sherehe hiyo.

Mwimbaji huyo alikaribishwa na jamaa na marafiki wa mzazi mwenzake Zari. Tiffah ambaye alikuwa hajui kinachoendelea alikuwa akicheza na marafiki zake wakati baba yake alingia chumbani.

Nilidhani hutakuja. Mama alisema hautakuja. Mama alidanganya,” Tiffah alisema huku baba yake akimnyanyua juu.

Malkia huyo mdogo ambaye hivi majuzi alifikisha umri wa miaka tisa alionekana kupigwa na butwaa alipokuwa akimkaribisha babake kwenye tafrija hiyo ya kifahari iliyohudhuriwa na familia na marafiki zake.

Video nyingine za tukio hilo zilimuonyesha Diamond akiimba wimbo wake maarufu ‘Komasava’ pamoja na watoto wake, akiwakabidhi zawadi na kutengeneza kumbukumbu nyingine nzuri nao. Mwimbaji wa WCB, D-Voice ambaye alikuwa ameambatana na bosi wake kwenye hafla hiyo pia alionekana akiwaburudisha wageni wakati tafrija ikiendelea.

Diamond alikuwa amebeba vitu vingi vya kuchezea pamoja na zawadi nyingine kwa ajili ya kuwasherehekea bintiye na mtoto wake wa kiume Prince Nillan, na walionekana kuzifungua kwa furaha.

Tiffah, ambaye ni binti wa staa huyo wa bongo fleva na sosholaiti kutoka Uganda Zari Hassan aligonga umri wa miaka 9 mnamo Agosti 6.

Zari alimsherehekea bintiye kwa kuchapisha picha zao nzuri wakiwa pamoja. Alimtaja msichana huyo wa miaka 9 kuwa ni Malkia wa Tanzania.

"Nisaidie kumtakia binti yangu wa pekee, Malkia wa Tanzania, siku njema ya kuzaliwa @princess_tiffah👗@hers_uganda," aliandika.