Muigizaji Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonie amesema muda utasema, kufuatia tukio la mzazi mwenzake, Mulamwah, kukutana kwa mara ya kwanza na binti yao Keilah Oyando baada ya muda mrefu.
Siku ya Jumapili, Mulamwah alipata nafasi adimu ya kutangamana na mtoto huyo wao wa miaka mitatu siku na wawili hao walionekana kuwa na wakati mzuri kulingana na picha zilizoonyeshwa na mchekeshaji huyo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Carrol Sonnie aliweka taarifa fupi akisema,“Muda utasema.”
Mkutano wa Mulamwah na binti yake Keilah unaaminika kuwa wa kwanza katika kipindi cha takriban miaka miwili, kulingana na madai ya hapo awali ya mchekeshaji huyo. Alikuwa amedai kuwa mzazi mwenzake alimzuia kuonana na binti yao, akisema mara ya mwisho kumuona alikuwa na umri wa miezi minne.
Katika posti zake za Jumapili, Mulamwah alionyesha picha na video nzuri zake akishiriki muda na bintiye na kuziambatanisha na emoji za moyo kuonyesha upendo.
Katika moja ya video alizochapisha, mchekeshaji huyo alionekana akicheza na binti yake na kumuonyesha jinsi ya kujiremba.
Keilah alizaliwa mnamo Septemba 2021, miezi michache tu kabla ya mchekeshaji huyo na mzazi mwenzake kutangaza kutengana. Wawili hao hata hivyo walikuwa wametengana miezi kadhaa kabla ya msichana huyo mrembo kuzaliwa.
Katika chapisho la mwezi uliopita, Mulamwah alidai kwamba alimuona binti yake mara ya mwisho akiwa na umri wa miezi minne pekee.
"Hakuna haja ya kwenda kwa Jeff na kusema 'Mulamwah ana uhusiano mzuri na binti yake. Hakuna uhusiano... Sijamwona binti yangu. Nilimwona mara ya mwisho akiwa na umri wa miezi minne. Usifunike ukweli,” Mulamwah alisema.
Mchekeshaji huyo aliongeza kuwa yuko tayari kurekebisha mambo.
”Mmenitumia barua za mkitaka mtoto awekwe chini ya ulezi wa mtu mmoja pekee lakini hapa nje ninaitwa baba asiyewajibika. Kuna mengi. Isipokuwa sisi sote tutarahisisha, kila kitu kitapita... Nitadrive niende kwao, sijaenda huko miaka mingi. Ukiniona na mtoto ujue mambo ni sawa, kama sivyo.....” alisema.