Isaac Wekesa Otesa, mwanamume mrefu kutoka kaunti ya Bungoma ambaye anasemekana kufanana sana na Bradley Marongo almaarufu ‘Gen-z Goliath’ ameomba kukutana na kijana huyo anayedaiwa kuwa pacha wake.
Katika mahojiano na Raipenda Evans, baba huyo wa watoto watatu alieleza jinsi alivyoshangaa baada ya kuona picha za Bradley zikivuma mitandaoni.
Isaac alieleza dhamira yake ya kujua kama kuna uhusiano wowote wa kindugu kati yake na Bradley, na hata akamkabili mama yake kwa maswali magumu.
“Mama, sasa vile huyo jamaa anasemekana yuko Nairobi, nami niko Bungoma, akisema niende mahali yuko ama yeye akuje Bungoma tuseme mimi ni ndugu yake, wewe utasema aje kama mzazi?” Isaac alimuuliza mama yake.
Bi Janet Wekesa ambaye alieleza waziwazi jinsi anavyojivunia mwanawe alibainisha kuwa yuko tayari kwa vipimo vyoyote kubaini iwapo wanaume hao wawili wana uhusiano wowote.
"Tutafuatilia, waende wapime kila kitu alafu tutajua," alisema.
Bi Janet hata hivyo alieleza imani yake kubwa kuhusu Isaac kuwa mwanawe wa kuzaa, akisema kwamba alimzaa nyumbani baada ya kukaa kwa miaka kadhaa kwenye ndoa bila mtoto.
“Yeye kuzaliwa, niko na wenye walinizalisha, na sikuzalia hospitali. Nilizalia tu nyumbani. Hata mimi mwenyewe sijawahi kufika huko Nairobi, sijawahi kwenda huko,” alisema.
Pia aliondoa shaka kwamba babake Isaka alitoka nje ya ndoa na kupata mtoto mwingine.
“Kusema yeye sio mtoto wangu, hiyo itakuwa ngumu kwangu. Mzaliwa wangu wa kwanza! Na hiyo miaka yote nimemaliza! Ninaweza kuita hata wenye waliniona na mimba, nikienda kliniki na nikizalia hapa nyumbani,” alisema.
Mamake Isaac pia alifichua kwamba baba ya mwanawe bado yu hai lakini hayupo nao kwa sasa.
Aidha, alisema kuwa mzazi mwenzake vile vile alishangaa sana alipoona picha za kijana anayefanana sana na mtoto wao zikivuma kwenye mitandao ya kijamii.
"Ata yeye vile aliona hiyo picha, alisema kweli Mungu anatenda kazi yake," alisema.
Mama huyo alibainisha kuwa kuna tofauti ndogo tu kati ya mwanawe na Bradley ambaye kwa sasa anaishi katika mtaa wa Kangemi, Nairobi.
Isaac alizaliwa katika kaunti ya Bungoma ilhali Bradley mwenye umri wa miaka 27 anatoka kaunti nyingine ya eneo la Magharibi, Bungoma.