Bi Janet Nekesa, mamake Isaac Otesa Wekesa, alikuwa mwanamke wa kuchekwa, kukejeliwa, na kudharauliwa kabla ya kujifungua mtoto huyo wake mrefu ambaye amepata umaarufu mkubwa hivi majuzi.
Isaac aliibuka hivi majuzi kwenye mitandao ya kijamii kufuatia madai kwamba anafanana na kijana Bradley Marongo almaarufu Gen-z Goliath ambaye pia alijipatia umaarufu kwa urefu wake mkubwa.
Katika mahojiano ya hivi majuzi na mwanahabari wa mtandaoni, Bi Janet alifichua kwamba alitatizika sana kupata mtoto katika miaka mitano ya kwanza katika ndoa yake kabla ya Isaac kuzaliwa.
“Nilibarikiwa na Isaac kama mtoto wangu wa kwanza, nilifurahia tena nikapenda Mungu kwa sababu sio rahisi kutenda jambo kama hilo. Ilikuwa tu maajabu, kama muujiza wa Mungu kwa sababu labda Mungu alitaka kujionyesha yeye ni Bwana,” Bi Janet alisimulia katika mahojiano na Raipenda Evans.
Aliendelea, “Kwa ndoa yangu nilipooleka, nilimaliza karibu miaka tano bila kupata mtoto. Nikawa wa kudharauliwa, nikawa wa kuchekelewa lakini nikamtegemea Mungu. Baada ya miaka tano, Mungu naye ni nani, nilibarikiwa nikaona nimepata mimba.”
Alisema kuwa alijifungua mtoto wake nyumbani na baadaye akaenda naye kliniki kwa uchunguzi.
“Alipozaliwa alikuwa kilo tano, mpaka wenye nilikuwa nao kwa boma wakashangaa, ata mama mkwe alishangaa huu ni muujiza tu,” alisema.
Bi Janet aliweka wazi kwamba alikuwa na furaha kwa kujifungua mtoto wake na kwamba alimlea vizuri bila matatizo mengi.
Alisema kuwa Isaac alikuwa mtoto mwenye afya njema na hakuwahi kuugua hadi alipokuwa na umri wa miaka kumi na tatu ambapo aliugua malaria kidogo.
“Nilimlea tu huku nyumbani Bungoma. Ukiangalia Isaac, ni Mungu tu alitaka aweze kusema jambo lisilo la kawaida. Amekuwa mtu mrefu, na mwili wak umekuwa mkubwae. Wenzangu walikuwa wakinitembelea wananiuliza nalisha nini mtoto?. Nilisema tu ni kazi ya Mungu,” alisema.
Mama ya Isaac alisema kwamba anafurahishwa na ukuaji wa mwanawe akibainisha kwamba amekomaa, amepata mke, na hata amemzalia wajukuu watatu.