"Kitu nilipata tu ni HIV!" Kisa cha kuhuzunisha cha mwanamke aliyeolewa na kuachwa mara 20, Akothee amfariji

Ndoa zote alizofunga hazikudumu hata hivyo, huku moja hata ikiisha baada ya wiki chache tu.

Muhtasari

•Bi Veronika anadai kuwa hakupata chochote kizuri kutoka kwa ndoa zake zote ishirini na aliishia tu kutalikiana na wanaume hao.

•Huku akimhurumia, mwimbaji Akothee aliwaomba watu kuwa wema kwa wengine kwani hawajui wamepitia nini.

amemfariji Bi Veronika ambaye anadai ameolewa na kupewa talaka mara 20.
Akothee amemfariji Bi Veronika ambaye anadai ameolewa na kupewa talaka mara 20.
Image: HISANI

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amemuhurumia mwanamke mzee ambaye amepitia masaibu si haba katika ndoa ishirini.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Akothee aliposti video ya mwanamke huyo aliyehojiwa kutoka mtaa wa mabanda wa Kibera, jijini Nairobi ambaye alikiri kuwa ameolewa na kupewa talaka mara ishirini.

Bi Veronica Okore, kama alivyojitambulisha, anadai kuwa hakupata chochote kizuri kutoka kwa ndoa zake zote ishirini na aliishia tu kutalikiana na wanaume hao. Pia alifichua kuwa aliambukizwa ugonjwa wa UKIMWI na sasa anatumia dawa.

“Katikati ya wanaume hao wote, mpaka huyo wa ishirini, nilipata tu ugonjwa wa HIV. Niko nayo nameza dawa. Na hiyo dawa siwezi meza bila kula,” Bi Veronica alisema.

Ajuza huyo mwenye umri wa miaka 71 ambaye sasa anaishi tu na mjukuu wake wa pekee katika mitaa ya mabanda ya Kibera baada ya kuachwa na watu wengine wote alifichua kuwa masaibu yake yalianza mwaka wa 1967 wakati babake alimuoza kwa mwanamume ambaye alimtafutia.

Alisema alikuwa mbali na nyumbani wakati mzazi huyo wake alipopanga na rafiki yake jinsi angeolewa.

Kwa bahati mbaya, ndoa yake haikuwa nzuri, hakuweza kupata mtoto na alitengana na mume wake wa kwanza baada ya miaka minne tu.

Baada ya kusambaratika kwa ndoa yake ya kwanza, Bi Veronica aliendelea kuolewa na wanaume wengine kumi na tisa huku akijaribu kutafuta yule wa kufaa kuwa na familia naye. Ndoa zote alizofunga hazikudumu hata hivyo,  huku moja ata ikiisha baada ya wiki chache tu.

Licha ya kufanya majaribu hayo yote ya ndoa, mwanamke huyo mkongwe bado yuko single na sasa anaishi kwa kujuta ikiwa yote aliyofanya yalifaa.

Huku akimhurumia, mwimbaji Akothee aliwaomba watu kuwa wema kwa wengine kwani hawajui wamepitia nini.

"Yoo, kuwa mkarimu kwa watu, hujui wamepitia nini hadi kuwa hapo walipo leo," Akothee alisema kupitia Instagram.

Aliendelea kumfariji mwanamke huyo na hata kuahidi kumtembelea hivi karibuni.

“Hapo pa kenye nilipata tu ni HIV.. Pole mama pole sanaa. Nitakuja kukutembelea hivi karibuni,” alisema