Kanyari anafaa kuomba msamaha kwa Wakenya kwa kumtania Mungu - Dr Ofweneke

Mchekeshaji huyo alisema kwamba Kanyari amekuwa na mazoea ya kutaka kutrend mitandaoni na kwa wakati uo huo anajikuta amefanya mzaha mpaka kwa vitu ambavyo havipaswi kutaniwa.

Muhtasari

• Hii si mara ya kwanza kwa Kanyari kusutwa kwa kauli zake za kukebehi na za kimzaha katika mitandao ya kijamii na haswa tangu alipojiunga katika mtandao wa video fupi wa TikTok.

PASTOR VICTOR KANYARI
PASTOR VICTOR KANYARI
Image: HISANI

 Mchekeshaji na mkuza maudhui kupitia mtandao wa YouTube Dr Ofweneke amemtaka mchungaji mwenye utata Victor Kanyari kuwaomba wakenya msamaha kwa kumdhihaki Mungu kwenye mimbari.

Akizungumza kupitia kipindi chake kwenye runinga ya TV47, Ofweneke alisema kwamba mchungaji huyo wa kanisa la Salvation Healing Ministry amekuwa akifanya mzaha kwa jina la Mungu pindi anaposimama kwenye madhabahu akiwamegea waumini wake injili.

Kwa mujibu wa Ofweneke, jinsi Kanyari alivyomshauri pasta Kiengei kumuomba msamaha mkuza maudhui Pritty Vishy kwa kudhalilisha maumbile yake, naye vile vile anastahili kuomba Mungu msamaha kwa kufanyia mchezo jina lake.

"Mimi mtu yeyote ambaye anamchukulia Mungu kwa mzaha, huyo huwa sina maneno mengi ya kuzungumza kumhusu. Kusema ukweli kama ambavyo pasta Kiengei ana deni la msamaha kwa Pritty Vishy, Kanyari pia ana deni la msamaha kwa Wakenya na jamii nzima ya Wakristo kwa kumkejeli Mungu, kukejeli madhabahu na kukejeli kila kitu kuhusu Mungu," Ofweneke alisema.

Mchekeshaji huyo alisema kwamba Kanyari amekuwa na mazoea ya kutaka kutrend mitandaoni na kwa wakati uo huo anajikuta amefanya mzaha mpaka kwa vitu ambavyo havipaswi kutaniwa.

"Ukweli usemwe, yeye [Kanyari] amekuwa akifanya chochote na ni sharti tumwambie ukweli hebu na tuwache kujikuta katika harakati za kutaka kutrend kwenye mitandao ya kijamii kwa kufanya mambo yanayomkasirisha Mungu. Trend wewe kama wewe na si kufanya vitu vya kumkejeli Mungu. Hiyo wachana nayo," aliongeza.

Hii si mara ya kwanza kwa Kanyari kusutwa kwa kauli zake za kukebehi na za kimzaha katika mitandao ya kijamii na haswa tangu alipojiunga katika mtandao wa video fupi wa TikTok.

Miezi kadhaa iliyopita, mchungaji huyo aliburuzwa mitandaoni baada ya kubainika kwamba aliwkaribisha watumizi wengine wa TikTok katika moja ya ibada ya kanisa lake.

Kanyari alifichua kwamba mmoja wa washawishi hao wa TikTok ambaye ni mwanamke alimpelekea zawadi ya kondomu.

Hili lilizua mtafaruku pevu si tu kutoka kwa Wakenya bali pia Wachungaji wenzake. Kwa mfano mchungaji T Mwangi alimsuta vikali akimtaja kama content creator na si mmoja wao.