Jalang’o atoa ushauri maalum kwa jamaa anayefanana naye kufuatia madai kwamba hamsaidii

Mbunge huyo alibainisha kuwa kufanana na mtu si kazi na akamtaka Mutisya atafute kitu cha maana cha kufanya.

Muhtasari

•Mbunge huyo wa Lang'ata alibainisha kuwa jamaa huyo anayejitambulisha kama Jalas Junior hamhitaji ili kujenga mafanikio.

•"Fanya kitu ungekuwa unafanya kama hufanani na mimi, kwa sababu na mimi sio kazi,” Jalang'o alishauri. 

Mbunge wa Lang'ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang'o na Jalas Junior
Image: HISANI

Mbunge wa eneo la Lang’ata Phelix Odiwour almaarufu Jalang’o ametoa ushauri maalum kwa mwanamume anayefanana naye, Stanley Mutisya, kuhusu jinsi anavyoweza kujijenga.

Akizungumza kwenye podcast ya Iko Nini, mtangazaji huyo wa zamani wa redio alibainisha kuwa jamaa huyo anayejitambulisha kama Jalas Junior hamhitaji ili kujenga mafanikio.

Jalang’o aliendelea kumhimiza kijana huyo kufanya chochote ambacho angekuwa anafanya ikiwa hangezaliwa akiwa kama yeye.

“Tuseme hakuwa anafanana na mimi. Afanye chenye angekuwa anafanya kama hakuwa anafanana na mimi. Unaona hiyo kitu ungekuwa unafanya na inakusaidia kama hungekuwa unafanana na mimi, wewe ifanye ikusaidie,” Jalang’o alimshauri Mutisya.

Mbunge huyo wa muhula wa kwanza alibainisha kuwa kufanana na mtu si kazi na akaweka wazi kuwa Mutisya anahitaji kutafuta kitu cha maana cha kufanya.

“Kufanana na mimi sio kazi. Unajua watu walimuuliza, wewe ungependa kufanya nini? Akasema mi naweza kufanya hivyo vitu Jalas alikuwa anafanya.. Anza, si lazima nikuwe ndio ufanye. Fanya kitu ungekuwa unafanya kama hufanani na mimi, kwa sababu na mimi sio kazi,” alisema.

Wiki chache zilizopita, Jalang’o alijibu kwa utani baada ya mwanamume huyo anayefanana naye kufanya mahojiano akilalamikia dhidi yake.

Jalas Junior, kama anavyojitambulisha kwenye mitandao ya kijamii, alilalamika kwenye mahojiano kuwa mtangazaji huyo wa zamani wa redio katika siku za nyuma aliahidi kumsaidia lakini hakuwahi kutimiza ahadi hiyo.

Blogu moja ya humu nchini ilichapisha mahojiano hayo kwenye mtandao wa Instagram na Jalang’o akajibu akisema kwamba hana jukumu la kumsaidia mtu kwa sababu tu anafanana naye.

“Mnajua nacheka nini? Hii ni maajabu! Yaani mkifanana sasa ukuwe wajibu wangu.. ungekuwa unafanana na mimi pia kwa kujituma na kutafuta haungefanya mahojiano haya!,” Jalang’o alijibu.

Mwanasiasa huyo aliendelea zaidi kuibua maswali kuhusu kazi ya kijana huyo akidokeza kwamba ‘kufanana na Jalas’ haiwezi kuwa kazi.

“Kwa hivyo ukiulizwa unafanya kazi gani kutafuta riziki.. Oooh nafanana na Jalas!” aliongeza.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, Jalas Junior alidai kuwa kitu pekee alichowahi kupata kutoka kwa mbunge huyo wa Lang’ata ni Ksh1000 baada ya kufanya naye mahojiano.

Alidai kuwa Jalang’o aliahidi kumsaidia baada ya mahojiano yao, lakini hajawahi kufanya hivyo licha ya yeye kumkumbusha mara kwa mara.

“Ujumbe wangu ni kumuuliza. Kwani alinidanganya?” Jalas Junior alihoji.

Kijana huyo amekuwa akionekana kwenye mitandao ya kijamii kwa muda sasa na amekuwa akifanya video za kumwiga mbunge huyo wa Lang’ata katika juhudi za kuunda maudhui.