"Naweza kuwa ndugu yako na hujui!" Jalas Junior amwambia Jalang'o huku akimuomba kazi

"Nadhani hutaki kunisaidia kwa sababu mimi sio Mjaluo, mimi ni Mkamba. Hiyo isikuzuie kunisaidia. Kwa saai nafanya kazi, najituma," Jalas Junior alisema.

Muhtasari

•Jamaa huyo anayejitambulisha kwa jina la Jalas Junior alibainisha kuwa tayari amefanya jitihada za kujitafutia riziki ya maisha.

•Amemuomba Jalang’o kupanga mkutano naye hivi karibuni na kutumia ushawishi wake kumsaidia kupata nafasi ya kazi.

Mbunge wa Lang'ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang'o na Jalas Junior
Image: HISANI

Stanley Mutisya, jamaa anayefanana na Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwour almaarufu Jalang’o amejibu baada ya mwanasiasa huyo kumshauri atafute kazi ya maana ya kufanya.

Akizungumza na waandishi wa habari za mitandaoni, mwanamume huyo anayejitambulisha kwa jina la Jalas Junior kwenye mitandao ya kijamii alibainisha kuwa tayari amefanya jitihada za kujitafutia riziki ya maisha.

Mutisya alimuomba mbunge huyo wa muhula wa kwanza kumsaidia bila kujali tofauti zao za kikabila akibainisha kuwa yeye pia ni mkazi wa eneo bunge la Lang’ata.

“Kusema ukweli nafanana na wewe. Nadhani hutaki kunisaidia kwa sababu mimi sio Mjaluo, mimi ni Mkamba. Hiyo isikuzuie kunisaidia. Mimi kwa saai nafanya kazi, najituma. Watu wa karibu ndio wanajua najituma. Pia nimesoma,” Mutisya alisema.

Alimwomba Jalang’o kupanga mkutano naye hivi karibuni na kutumia ushawishi wake kumsaidia kupata nafasi ya kazi.

Katika ombi lake, kijana huyo alibainisha  kuwa kuna uwezekano kwamba yeye na mwanasiasa huyo wana uhusiano wa damu.

“Mimi ni mtu wa Lang’ata. Toa hiyo fikra ya ati wewe ni Mjaluo huwezi kusaidia Mkamba. Huwezi jua, mimi naweza kuwa ndugu yako na hujui. Naweza kuwa ndugu yako wa kweli. Pia mimi najituma, nafanya kazi. Mheshimiwa ingilia kati unitoe block,” aliomba.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Jalang’o kujitokeza kwenye podikasti ya Iko Nini ambapo alimshauri Mutisya kutafuta kazi ya maana ya kufanya.

Katika kipindi hicho, mtangazaji huyo wa zamani wa redio alibainisha kuwa jamaa huyo anayejitambulisha kama Jalas Junior hamhitaji ili kujenga mafanikio.

Jalang’o aliendelea kumhimiza kijana huyo kufanya chochote ambacho angekuwa anafanya ikiwa hangezaliwa akiwa kama yeye.

“Tuseme hakuwa anafanana na mimi. Afanye chenye angekuwa anafanya kama hakuwa anafanana na mimi. Unaona hiyo kitu ungekuwa unafanya na inakusaidia kama hungekuwa unafanana na mimi, wewe ifanye ikusaidie,” Jalang’o alimshauri Mutisya.

Mbunge huyo wa muhula wa kwanza alibainisha kuwa kufanana na mtu si kazi na akaweka wazi kuwa Mutisya anahitaji kutafuta kitu cha maana cha kufanya.

“Kufanana na mimi sio kazi. Unajua watu walimuuliza, wewe ungependa kufanya nini? Akasema mi naweza kufanya hivyo vitu Jalas alikuwa anafanya.. Anza, si lazima nikuwe ndio ufanye. Fanya kitu ungekuwa unafanya kama hufanani na mimi, kwa sababu na mimi sio kazi,” alisema.