Kajala ajibu baada ya Stevo Simple Boy kukiri kummezea mate, kumuomba awe mkewe

Muigizaji Kajala Masanja alijibu kwa njia ya utani baada ya rapa Stevo Simple Boy kukiri upendo wake mkubwa kwake.

Muhtasari

•Stevo alichapisha video akizungumzia jinsi anavyompenda mpenzi  huyo wa zamani wa Harmonize na akasifia urembo wake.

•Huku akijibu video hiyo, Kajala alibaini kuwa mwimbaji huyo alimuita ‘mtoto parachichi’ na anashangaa kwa nini hivyo.

amekiri upendo wake kwa Kajala Masanja
Stevo Simple Boy amekiri upendo wake kwa Kajala Masanja
Image: HISANI

Muigizaji wa Tanzania Frida Kajala Masanja alijibu kwa njia ya utani baada ya rapa wa Kenya, Stevo Simple Boy kukiri upendo wake mkubwa kwake.

Siku ya Jumamosi Stevo alichapisha video akizungumzia jinsi anavyompenda mpenzi  huyo wa zamani wa Harmonize na akasifia urembo wake.

Huku akijibu video hiyo, Kajala alibaini kuwa mwimbaji huyo alimuita ‘mtoto parachichi’ na anashangaa kwa nini hivyo.

“Kwa nini parachichi?” Kajala aliandika na kusindikiza kauli yake yenye emoji za uso unaocheka.

Siku ya Jumamosi, rapa huyo anayeishi Kibera kupitia ukurasa wake wa Instagram alichapisha video iliyomuonyesha akipika mlo wa samaki.

Katika video, alieleza kuwa licha ya kwamba alikuwa akifanikiwa kupika mwenyewe, alitamani sana Kajala angekuwa anampikia.

Napika chakula zangu hapa. Lakini nikipika naona tu katoto fulani kanaitwa Kajala,” Stevo alisema kwenye video hiyo.

Mwimbaji huyo aliendelea kukiri upendo wake mkubwa kwa mama huyo wa binti mmoja na kusifu uzuri wake unaoonekana.

“Kajala, Kajala Kajala, mazee mi nimedata kwako, na tena umenivutia. Kajala tafadhali njoo unipikie, unioshee vyombo, unipangie nyumba,” alisema.

Aliongeza, “Mi nakwambia Kajala mtoto wa lombolombo, mtoto kamirigado, mtoto parachichi, mtoto gudaguda, mtoto amebeba ngogingo. Mtoto ako checheche. Mtoto mwah mwah mwah. Kajala mi nakwambia nakupenda.

Haya yalijiri wakati mwimbaji Stevo Simple Boy anaaminika kuwa single baada ya kutengana na aliyekuwa mke wake, Grace Atieno.

Hali ya uhusiano ya Kajala hata hivyo kwa sasa haijulikani kwani amejaribu sana kuweka mambo kuwa siri tangu alipotengana na staa wa bongofleva Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize.

Kajala alimtema Kondeboy tariban miaka 2 iliyopita baada ya kuchumbiana kwa miezi kadhaa. Mastaa hao walikuwa wamerudiana Mei 2022 baada ya kutengana mwaka mmoja.

Wakati akitangaza kuachana na mwanamuziki huyo mwezi Desemba 2022, Kajala aliweka wazi kwamba alikuwa tayari kupiga hatua nyingine baada ya mahusiano yao ya miezi michache kugonga mwamba.

Ingawa hakufichua kilichowatenganisha, aliweka wazi kwamba hakubeba kinyongo chochote dhidi ya mwimbaji huyo.

"Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema wakat huo.

Wakati wa mahojiano na kituo cha redio cha hapa nchini mapema mwaka huu, Kajala alidokeza kuwa alimtema Harmonize kwa sababu ya mazoea.

"Sijui niseme nini. Labda mazoea. Mtu akishakuzoea sana anakuchukulia poa," alisema.