Bungoma Goliath afunguka sababu ya kutoroka Nairobi kurudi nyumbani

Pia alidai kuwa hakukuwa na chakula bora mahali ambapo alikaribishwa jijini Nairobi

Muhtasari

•Isaac anasema baada ya kufika Nairobi alipelekwa kwenye nyumba ambapo alilazimika kulala kitanda kimoja na watu wengine wawili.

•Pia anasema hakupenda mambo ambayo alikuwa akishauriwa kuyafanya na watu waliokuwa naye ili kujipatia umaarufu.

Isaac Otesa
Image: HISANI

Isaac Otesa Wekesa, mwanamume mrefu kutoka kaunti ya Bungoma amefunguka kuhusu kwa nini aliamua kurejea nyumbani baada ya kuwa jijini Nairobi kwa siku chache tu.

Katika mahojiano na IkuweIkuwe, jamaa huyo anayetambulika kama Bungoma Goliath kwenye mitandao ya kijamii alibainisha kuwa alifunga safari ya Nairobi baada ya kushawishiwa na mashabiki.

Isaac alifichua kwamba alipokuwa akiondoka Bungoma, alikuwa ameahidiwa kupelekwa kwenye mahojiano katika kituo kimoja cha televisheni maarufu nchini Kenya, jambo ambalo halikutimia.

Alisema badala yake alipelekwa kwenye nyumba ambayo alilazimika kulala kitanda kimoja na watu wengine wawili, hali ambayo aliiona kuwa haiwezi kuvumilika na kumfanya aondoke.

“Hiyo haikunifurahisha, kulala mwanamke na wanaume wawili kwa kitanda moja. Ndio nikatoka nikaenda kwa mashemeji zangu huko Nairobi,” Isaac alisema.

Pia alidai kuwa hakukuwa na chakula bora mahali ambapo alikaribishwa jijini Nairobi, na kulikuwa na ahadi nyingi alizopewa ambazo hazikutimizwa kamwe.

Baada ya kuwa Nairobi kwa muda, anasema aliombwa aanze kusaidia katika kununua chakula kwa kutumia pesa kidogo alizopata.

“Ile kidogo nilikuwa nimepata ambayo nilitaka nisaidie watu nyumbani na nilipie pikipiki, niliambiwa nisaidie kununua chakula. Sasa nikaanza kununua chakula, nikaona ni ngumu. Ndio maana nikatoka,” alisema.

Sababu nyingine iliyomfanya mwanaume huyo mrefu kutoka Bungoma kuamua kurejea nyumbani ni mambo ambayo alikuwa akishauriwa kuyafanya na watu waliokuwa naye ili kujipatia umaarufu.

Isaac anasema kwamba alishauriwa kumkalia mwanamke na kucheza densi naye, na pia kulala kitanda kimoja naye kwa jina kutafuta kiki.

“Sikuwa najua vitu hivyo kwa sababu sijawahi fanya hivyo. Ilikuwa mara ya kwanza. Ndio nikasonga ili kuepuka vitu hivyo kwa sababu niliona kuwa zinafurahisha mashabiki,” alisema.

Isaac alikuwa amefunga safari kutoka Bungoma hadi Nairoi wiki chache zilizopita akiwa na matumaini ya kupata mambo mazuri jijini.

Hata hivyo alionekana akirejea nyumbani katika eneo la Magharibi mwa Kenya baadaye baada ya kuwa katika mji mkuu kwa siku chache.