"Pole Jared" Akothee, binti zake wamfariji aliyekuwa mumewe huku akimzika kakake

Akothee aliandamana na mamake pamoja na binti zake Vesha Okello na Rue Baby kwenye hafla hiyo iliyofanyika Homa Bay.

Muhtasari

• Akothee alichapisha video ya Jared akitoa hotuba ya huzuni na katika sehemu ya maelezo, akamfariji mumewe huyo wa zamani.

“Imenisambaratisha, imenivunja. Lakini ninataka kuwashukuru marafiki zangu ambao wamesimama nasi,” Jared alisema.

Akothee na aliyekuwa mumewe, Jared Okello katika picha ya maktaba.
Akothee na aliyekuwa mumewe, Jared Okello katika picha ya maktaba.
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Siku ya Alhamisi, mwimbaji na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee alihudhuria mazishi ya jamaa wake aliyefariki hivi majuzi.

Mama huyo wa watoto watano aliandamana na mamake pamoja na binti zake wawili wakubwa, Vesha Okello na Rue Baby kwenye hafla hiyo iliyofanyika katika kaunti ya Homa Bay.

Marehemu David Odhiambo Otieno ambaye ni kakake aliyekuwa mume wa Akothee Jared Okello, alipoteza maisha mnamo Septemba 6, 2024 na siku ya Alhamisi, mwimbaji huyo aliamua kujiunga na familia ya baba ya binti zake watatu katika kumzika mpendwa huyo.

Wakati akiwa kwenye mazishi, Akothee alichapisha video ya Jared akitoa hotuba ya huzuni na katika sehemu ya maelezo, akamfariji mumewe huyo wa zamani.

“Pole Jared,” Akothee aliandika.

Katika video iliyochapishwa na Vesha, Bw Jared alisikika akizungumzia jinsi alivyovunjika moyo baada ya kupoteza wanafamilia kadhaa kwa muda mfupi.

“Imenisambaratisha, imenivunja. Lakini ninataka kuwashukuru marafiki zangu ambao wamesimama nasi,” Jared alisema.

Vesha pia alichapisha video nyingine inayoonyesha kaburi la marehemu David na kuitakia roho yake amani ikipumzika.

“Pumzika kwa amani mjomba, naweza nisielewe lakini ni sawa,” vesha aliandika.

Mapema mwezi huu, Akothee alimwandikia barua ya kihisia marehemu shemeji yake David Odhiambo ambaye alidaiwa kujitoa uhai

Katika barua yake, Akothee alimhurumia marehemu shemejiye lakini akakosoa uamuzi wake wa kujitoa uhai na kuacha familia yake nyuma.

Msanii huyo alibainisha kuwa uamuzi wa mwanamume huyo umewaacha wengi na mioyo iliyovunjika ikiwa ni pamoja na watoto wake mwenyewe.

“Mpenzi Shemeji, sina nguvu ya kukuhukumu kutokana na uamuzi ulioufanya wa kumaliza safari hii. Huenda nikataka kuuliza kwa nini hukuwasiliana nami au hata kwa wapwa zako, lakini labda ulifikiri kila mtu alishikwa na matatizo yake,” Akothee aliandika kwenye Instagram.

Aliambatanisha barua yake na picha za kumbukumbu za shemeji yake.

”Lakini sasa, niruhusu nikuulize—vipi kuhusu mke wako na watoto wako? Omuga na wengine? Daudi, je, hukumfikiria mama yako, ambaye amekuwa mjane mwaka mmoja uliopita? Kwa nini ukawa mbinafsi sana, Odebi? Umevunja mioyo ya watoto wangu,” aliongeza.

Mama huyo wa watoto watano pia aliomba msamaha kutoka kwa marehemu na kubainisha kuwa wameachwa katika huzuni.

“Samahani sana, Odebi. Utusamehe kwa kutokuwepo kwa ajili yako, lakini kusema kweli, sote tumekasirika na maisha haya sasa, sote tunaondoa vichwa vyetu majini ili tu kuepuka kukosa hewa,” Akothee alisema.

"Pumzika kwa amani, Omejo.Yuora ma ok luonga gi nyinga," aliongeza.