Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amefunguka kuhusu kutengana kwake mara kadhaa na mpenzi wake Nelly Oaks.
Katika taarifa yake siku ya Jumapili, mama huyo wa watoto watano aliweka wazi kuwa hajawahi kumkosea mwanamume huyo ambaye pia ni meneja wake katika uhusiano wao wa takriban muongo mmoja.
Akothee alisema, tofauti na jinsi watu wengi wanavyofikiri, Nelly ndiye amekuwa akianzisha migogoro na kuachana kwao katika miaka kumi waliyotoka kimapenzi.
"Hakuna mwanamke atakayeacha uhusiano mzuri. Naona wengi mnadhani mimi ndiye ninayemchukua na kumtema Nelly, lakini wacha nianze mwaka kwa ukweli. Ni yeye ambaye kila mara amekuwa akianzisha vita vyetu na kuachana,” Akothee alisema kupitia mtandao wa Instagram.
Aliongeza, “Kama mwanamke, ninapofikia kikomo, ninachagua kuondoka na kuishi maisha yangu, kwa sababu, nina maisha ndani ya maisha tuliyo nayo. Tunaenda kwa njia zetu tofauti na kuzingatia njia zetu wenyewe, lakini changamoto ni uhusiano thabiti kati yetu.
Msanii huyo aliendelea kuzungumza juu ya kile kinachotokea kila wanapoachana.
“Kila tunapoachana huwa nam’block na kufuta namba yake, lakini njia zetu zikivukana tena tunashika pale tulipoishia. Usikose: Mimi ni mshirika mwaminifu, wa kweli, na mwenye upendo," alisema.
Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alisisitiza kwamba yeye huwa katika uhusiano mmoja kwa wakati mmoja na huwa hachumbii zaidi ya mwanamume mmoja kwa wakati mmoja.
Aidha, alisisitiza kwamba inachukua juhudi za wapenzi wote wawili kufanya uhusiano ufanyike.
“Nampenda kwa uaminifu wangu wote. Mimi ni mwanamke ninayechumbiana na mwanamume mmoja mmoja,” alisema.
Wawili hao wamekuwa wakichumbiana kwa muda mrefu sasa.
Hapo awali waliwahi kuachana mara kadhaa, huku Akothee hata akichukua hatua ya kuolewa na mwanamume mwingine mwaka jana, lakini hatimaye walirudiana na kuendelea na uhusiano wao.