Msanii wa mizki ya kizazi kipya kutoka humu nchini, Otile Brown amechukua kwenye ukurasa wake wa Instagram kutamka shukrani zake kwa shabiki wake kutoka Marekani aliyemtumia zawadi ya kipekee.
Otile alimtaja shabiki huyo wa kike na kumshukuru kwa kumtumia zawadi ya simu aina ya iPhone 16, akisema kwamba hawezi kujihisi mwenye fahari zaidi ya hapo.
“Ahsante sana malkia kwa zawadi ya iPhone 16.Umefana siku yangu na Mungu akubariki,” aliandika kwenye video fupi aliyoichapisha kwenye instastory yake.
Akijisifu jinsi muziki wake umeleta athari chanya kwa mashabiki wake wengi kutoka kila kona ya dunia, Brown alifichua kwamba shabiki huyo alimtumia zawadi hiyo kama kifurushi moja kwa moja kutoka Marekani.
“Shukrani za dhati shabiki wangu kutoka Marekani kwa zawadi hii na hii inaonyesha jinsi nilivyo na mashabiki kutoka pande zote za dunia. Hii ni simu yangu ya pili ambayo nimezawadiwa na shabiki na nakuambia nina mashabiki wazuri zaidi duniani. Si jambo la kawaida msanii kufanyiwa vitu kama hivi na ningependa kusema tu ahsante,” aliongeza kwa furaha.
Hii si mara ya kwanza kwa msanii huyo kuonyesha zawadi ya simu aliyopokezwa kutoka kwa shabiki wake.
Mnamo Julai 2023, Brown alionyesha zawadi ya simu ya iPhone 14 akisema kwamba ilitoka kwa shabiki wake mmoja, siku chache baada ya kampuni ya Apple kuzindua simu za iPhone 14.