Esther Musila, mke mwanamuziki wa nyimbo za injili Guardian Angel ameeleza ni kwa nini aliwacha kazi yake ya benki na
kukaa nyumbani.
Kwa mazungumzo ya podikasti ya bintiye Gilda Naibei, Esther Musila alielezea sababu ya yeye kuwacha kazi yake ya benki na kuchagua kukaa nyumbani akilea watoto wake.
Musila alifichua kwamba alipata ujauzito wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 19 na wa mwisho akiwa na umri wa miaka 28.
Anasema kwamba alikuwa na ndoto ya kuolewa na kuwa na familia atakapofikisha umri wa miaka 26 kwani alikuwa na matumaini ya kupata kazi nzuri na kuweza kujitegemea lakini mambo hayakuenda alivyopanga kwani alipata ujauzito mapema kinyume na matarajio.
“Nilipokuwa nakuwa, ni wazi nilikuwa na matarajio yangu sababu nakumbuka niliwahi kusema nitaolewa nikiwa na miaka 26. Na nilikuwa na matumaini kuwa mpaka hapo nitakuwa nimeshapata kazi nzuri, nimekuwa stable au kuhitimu maishani mwangu, basi nitaanzisha familia,"
Alipoulizwa kama alikuwa amepanga kuolewa akiwa na umri mdogo, Musila alisema kwamba ni jambo ambalo hakuwa amepanga kwani mimba ya mapema ndio ilisababisha hayo.
"Siwezi kusema kwamba nilipanga kuoa, ilitokea tu nilipokutana na mtu...Kwangu sikupanga nilikutana na mtu kitu kinachofuata nadhani uhusiano kidogo alafu una mimba ya mtoto wa kwanza na nikaona sasa ni wakati wa mimi kuanza maisha,” Musila aliendelea na kusema kwamba hofu ya watoto wake kupelekwa shule na mtu mwingine ndiyo sababu ya yeye kuwacha kazi yake ya benki na kwenda kukaa nyumbani kulea wanawe. “Sababu iliyonifanya niamue kukaa nyumbani ni kwa sababu nilikuwa na nyie wawili na mlikuwa na tofauti ya miaka 3 alafu mkaanza kwenda shule, mmoja anaenda kinyume na mwingine. Na nadhani mimi kuwa na woga wa watoto wangu kupelekwa shuleni na mtu mwingine iliniletea hofu kidogo. Kwa hivyo niliamua kwa sababu watoto hawa ni wachanga, wacha niwache kazi. Bosi wangu aliogopa sana kwa sababu nilikuwa na miaka 26 na ninafanya kazi benki, na aliniuliza ‘ una umri wa miaka 26 unaenda wapi?’ Kwa hiyo niliamua nijinyime kazi yangu kwa kipindi fulani ili niwalee watoto na kwangu hilo liliniridhisha zaidi kwa sababu nilimpeleka kila mmoja wenyu shuleni,” alisema. Baadaye alipata mtoto wake wa tatu akiwa na umri wa miaka 28.