Seneta wa kaunti ya Nandi Samson Cherargei amefutilia mbali
nia ya aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang’I kuwania urais katika uchaguzi
mkuu ujao wa mwaka 2027.
Kauli ya seneta Cherargei inajiri baada ya taarifa kusambaa
kuwa waziri huyo wa zamani amekodi huduma ya waajuzi wa maswalaya uchaguzi
waliohusika katika uchaguzi uliokamilika nchini Botswana ilikumsaidia katika
azma yake ya kuwa rais katika uchaguzi mkuu ujao.
Kwa mujibu wa Cherargei, amemsuta Matiang’I akisema kuwa
chini ya hatamu yake kama waziri katika utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta,
visa vya mauaji ya kiholelela, mateso ya kisiasa na kupotea kwa watu kwa lazima
kulitukia mno na ilikuwa ratiba ya kila siku.
Kwa mujibu wa gazeti moja la Kenya, Matiang’i ametia sahihi
katika mkataba na kampuni iliyohusika pakubwa na ushindi wa Duma Boko katika
uchaguzi wa Botswana uliofanyika Oktoba 30.
Seneta Cherargei amesema kuwa Fred Matiang’i hawezi kumbandua
rais William Ruto katika uchaguzi ujao
akidai kuwa waziri huyo wa zamani hawezi ata kuchaguliwa kusimamia josho
nyumbani kwao katika kaunti ya Nyamira.
“Nabashiri kuwa hawezi ata kuchaguliwa kama mwenyekiti wa josho mahali
popote ndani ya Nyamira.” Alisema Cherargei.
Seneta huyo pia amesema kuwa wakati wa Matiang’i kama waziri
wa maswala ya ndani ndipo mili ya watu ilipatikana katika mbuga ya Tsavo na mto
Yala.
Hata hivyo Matiang’i hajatangaza rasmi nia ya kuwania urais
wa Kenya katika mwaka wa 2027.