Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amethibitisha kuwa ni kweli kuna mzozo unaozingira nyumba yake ya kukodi katika mtaa wa Runda, kaunti ya Nairobi.
Katika mahojiano na mwanahabari Sarah Ibrahim, mama huyo wa watoto watatu hata hivyo alipuuzilia mbali madai kwamba amefilisika na hawezi kulipa kodi.
Nyamu alifichua kuwa kuna mzozo kati yake na mwenye nyumba lakini akabainisha kuwa vitu vyake vya nyumba bado havijapigwa mnada.
“Mshahara wangu wenyewe ni milioni 1.2. Ikiwa sijalipa kodi, au kama kuna mzozo wowote, sio kwa sababu sina pesa,” Karen Nyamu alisema.
Aliongeza, "Mizozo hutokea, katika kila hali. Inaweza kuwa kati ya bosi na mfanyakazi, inaweza kuwa marafiki. Ni kweli, kuna mzozo. Lakini sijasota.”
Mwanasiasa
huyo aliyezingirwa na utata mwingi aliweka wazi kuwa yeye hazitumii pesa zake vibaya
au kuzichezea kamari.
Pia alibainisha kuwa serikali imewapa maseneta rehani nzuri ili kupata nyumba zao.
“Niko sawa, sijapigwa mnada. Lakini kuna mzozo kidogo hapo nitatatua,” alisema.
Aidha, Bi Nyamu alidokeza kuhusu uwongo katika madai ya kupigwa mnada na akakosoa kitendo cha kuanika jina lake kwenye vyombo vya habari.
Haya yanajiri siku chache baada ya ripoti kuibuka kuwa madalali wanafuatilia vitu vya nyumbani vya mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata kuhusu madai ya malimbikizo ya kodi ya Ksh1.25milioni.
Siku ya Jumatatu, iliripotiwa kuwa, amri ya mahakama iliyotolewa na Hakimu Mwandamizi wa Milimani A.H. Nyoike mnamo Novemba 13, 2024, ilionyesha kuwa seneta Nyamu yuko hatarini kupigwa mnada ili kurejesha kiasi cha kodi ambacho hakijalipwa.
Kulingana na amri ya korti, kiasi hicho kingerejeshwa na Fantasy Auctioneers kwa niaba ya mwenye nyumba.
Mahakama
pia iliagiza Kituo cha Polisi cha Runda kuweka ulinzi kwa madalali hao.
"Ofisa anayesimamia Kituo cha Polisi cha Runda au afisa mwingine yeyote aliye chini ya amri yake atoe msaada kwa madhumuni ya kudumisha sheria na utulivu," ilisomeka amri ya mahakama.
Seneta Nyamu hata hivyo amepinga hatua ya vitu vyake vya nyumbani kupigwa mnada.
Vitu vilivyolengwa viko nyumbani kwa mwanasiasa huyo katika Graceville Villas, mtaa wa Runda.